Tarehe : Jan. 28, 2018, 5:19 p.m.
Na Nuru Mwasampeta,
Waziri wa Madini Doto Biteko, amewataka Maafisa Madini wa mikoa kuepuka tuhuma za rushwa na urasimu na kubainisha kuwa, hatamfumbia macho Mtumishi yeyote atakayebainika kutekeleza majukumu yake kinyume na Sheria.
Aidha, amewataka maafisa hao kuwabaini na kuwatambua wachimbaji wadogo waliopo katika maeneo yao ya kazi.
Biteko aliwaeleza maafisa hao kuwa wizara haita mfumbia macho mtumishi yeyote asiyetekeleza majukumu yake na kukiri kuwa ni vema kufanya kazi na watu wachache kuliko kufanya kazi na mamia ya watu wasiokidhi mahitaji na kasi ya wizara katika kutekeleza majukumu yao.
Biteko alitoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki alipofanya mkutano baina yake, Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Simon Msanjila, Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na maafisa Madini wa Mikoa. Mkutano huo uliolenga kutoa msisitizo katika kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji na wafanyabiashara wa madini katika maeneo yao ya kazi.
“Tunao wachimbaji wadogo wengi, wengi sana. Walio rasmi na wasio rasmi. Mwenye wajibu wa kuwatambua wachimbaji hao ni ninyi. Lazima sasa hivi mkatengeneze data base kwenye mikoa yenu ili kujua akina nani wanajihusisha na shughuli za uchimbaji mdogo ili tutakapotaka kuwasaidia wachimbaji wadogo misaada hiyo itolewe kwa wahusika kuliko kubahatisha,” alisisitiza Biteko.
[ Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao baina ya uongozi wa wizara na Maafisa Madini wa Mikoa kilichofanyika katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam
“Tunataka kuanzisha soko la madini, na Serikali itatoa nafuu (incentive) kwa wachimbaji wadogo, nafuu kwenye kodi, nafuu kwenye ushuru, sasa hawa wachimbaji wadogo watakaonufaika na punguzo hilo lazima tuwajue ni akina nani, lazima tuwe pro- active katika utendaji wetu wa kila siku” alikazia.
Aidha, Waziri Biteko aliwataka Maafisa hao kwenda kutekeleza na kusimamia Sheria na kukataa kila aina ya maelekezo yanayotolewa kwao ambayo yanayokiuka sheria katika utekelezaji wa majukumu yao.
Biteko aliongeza kwa kuwataka Maafisa madini wa mikoa kuhakikisha wanafanya kazi na kulifanya jina la Wizara ya Madini linakuwa zuri kuliko kuonekana kama watu wasiokuwa na mwelekeo wa kiutendaji.
Biteko alibainisha kuwa mpaka sasa wizara imehamisha watumishi 57 makao makuu ya wizara ambao wizara imejiridhisha kuwa utendaji kazi wao hauridhishi na kwamba zoezi hilo litaendelea kwa lengo la kuimarisha utendaji wizarani.
Zaidi ya hayo, Biteko aliwataka Maafisa Madini hao kuhakikisha kuwa wanashirikiana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuwataka kuwajibika kwao kwani ni wawakilishi wa Rais na wanasimamia shughuli za Serikali.
Aliongeza kuwa, wakuu wa wilaya ni wasimamizi wa Serikali katika maeneo hayo, ni wawakilishi wa Rais katika wilaya na mikoa hiyo ni wasimamizi wa kazi zote za serikali ikiwepo ya madini hivyo hawana budi kushirikiana nao.
Biteko aliwataka maafisa Madini hao kuwasilisha changamoto wanazokutana nazo ziwe ni za kibajeti au vifaa ili waweze kusaidiwa na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao na kuwaagiza kumtumia Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Simon. Msanjila katika kutatua changamoto hizo.
Akizungumzia suala la uanzishwaji wa vituo vya madini katika mikoa. Biteko alisema, Kanuni za kusimamia vituo hivyo zimekwisha andaliwa na zitasainiwa wakati wowote na kuwataka maafisa hao kutambua kuwa wao ni watu muhimu katika kusimamia vituo hivyo.
Biteko alisema anatamani ndani ya miezi sita sekta ya madini ibadilike, mtu akija aone kuna maendeleo, aliwasihi kuhama kwenye majina ya kuitwa wala rushwa, tuhame kuitwa warasimu tuhame kwenye sifa za watu wanaosimamia masuala ya madini pamoja na kujihusisha na shughuli za uchimbaji jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Akihitimisha kikao hicho, Biteko aliwataka maafisa hao kuhakikisha mapendekezo yote yaliyotolewa katika mkutano wa kisekta kila mtu katika mkoa wake akayafanyie kazi. Pia aliwaagiza kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi wa wizara kwa nyakati tofauti ikiwa ni pamoja na yale yaliyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Tume ya Madini, Prof. Shukrani Manya alieleza kufurahishwa na kukiri kwenda kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na kiongozi wa wizara hiyo.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.