Tarehe : April 28, 2018, 12:50 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewaahidi wananchi wa Kagera kuwa Serikali inashughulikia kwa umuhimu mkubwa na kwa haraka suala la Soko kwa ajili ya Madini ya Bati yanayochimbwa wilayani Kyerwa, ili waendelee kunufaika nayo na nchi ipate faida kama ilivyo kwa majirani zetu wa Uganda na Rwanda.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu (katikati), akisoma Taarifa ya Sekta ya Madini ya Mkoa huo, mbele ya Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia kwake), alipomtembelea ofisini kwake akiwa katika ziara ya kazi Februari 27 mwaka huu.[/caption]
Alitoa ahadi hiyo jana, Februari 27 ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo, Meja Jenerali (Mstaafu) Salum Kijuu, akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kazi mkoani humo.
Akizungumza na Mkuu wa Mkoa pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Naibu Waziri Nyongo alikiri kuwa wachimbaji wa Madini ya Bati hapa nchini, kwa sasa wana wakati mgumu kutokana na Serikali kusitisha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi; hata hivyo akasema kuwa hali hiyo itakoma hivi karibuni kwa kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa haraka.
Akifafanua zaidi, Nyongo alisema kuwa Tanzania ilichelewa kujiunga na Mkataba wa Kimataifa unaowezesha madini hayo kutambuliwa na kununulika kokote, hali iliyosababisha nchi jirani za Rwanda na Uganda ambazo zimeshajiunga na Mkataba huo, kutumia fursa hiyo kununua malighafi hiyo muhimu kutoka kwa wachimbaji wa hapa nchini kwa bei ya chini sana.
Alisema kuwa, ni kwa sababu hiyo Serikali iliamua kusitisha uuzaji wa madini ghafi nje ya nchi mpaka pale itakapokamilisha taratibu mbalimbali zitakazoiwezesha nchi na wananchi wote kunufaika ipasavyo kutokana na madini mbalimbali yanayopatikana nchini, ikiwemo kuharakisha mchakato wa kujiunga na Mkataba huo wa Kimataifa.
“Kwa hiyo, mimi nikuhakikishie kwamba, suala hilo tunalishughulikia kwa uharaka ili kuhakikisha nasi kama kama nchi tunatambulika katika Mikataba hiyo ya Kimataifa, ili nasi tuanze kuuza Bati yetu vizuri. Tunalichukulia suala hili kwa umuhimu wa kipekee.”
Aidha, Nyongo aliieleza pia Kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama kuhusu suala la utoaji Leseni za Madini nchini, kwamba utaendelea mapema iwezekanavyo mara tu baada ya Tume ya Madini itakapoanza kufanya kazi.
“Tume itaanza kufanya kazi muda wowote kuanzia sasa, mara tu Mheshimiwa Rais atakapofanya uteuzi wa Mwenyekiti wake. Na itakapoanza kazi tu, zoezi la utoaji na uhuishaji wa Leseni litaendelea.”
Mjiolojia Samwel Shoo, kutoka Ofisi ya Madini Kagera (kushoto) akimwonesha Naibu Waziri Stanslaus Nyongo, aina mbalimbali ya sampuli za madini yanayopatikana mkoani Kagera humo. Naibu Waziri alitembelea Ofisi ya Madini akiwa katika ziara ya kazi mkoani Kagera, Februari 27 mwaka huu.[/caption]
Vilevile, alifafanua kuwa, kufuatia kufutwa kwa iliyokuwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na kuundwa Tume ya Madini; hakutakuwa tena na Ofisi za Madini za Kanda bali kutakuwa na Ofisi za Madini za Mikoa.
Kwa upande wa Madini ya Nickel ambayo pia yanachimbwa ndani ya Mkoa huo, Naibu Waziri alisema kuwa ni moja ya madini yanayoleta matumaini mapya ya kulinufaisha Taifa kutokana na umuhimu wake katika Soko la Dunia kwa sasa.
Alisema kuwa, kutokana na kukua kwa Teknolojia Duniani, Madini ya Nickel yanahitajika sana, hususan katika nchi zilizoendelea kwa ajili ya kutengeneza Betri maalum za Magari ambazo zinachajiwa na hivyo kutotumia mafuta.
“Sasa hivi nchi zilizoendelea wanataka kupunguza matumizi ya mafuta kwenye magari na ukienda Miji mikubwa ya Ulaya, wanataka kufikia 2040 wasitumie tena mafuta kwenye Magari yao, badala yake watumie Betri. Nickel ni madini muhimu sana katika utengenezaji wa Betri hizo na mitambo mingine inayohifadhi chaji za umeme kama vile kwenye Simu na kadhalika.”
Kuhusu uwekezaji katika Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold, unaomilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Naibu Waziri alieleza kuwa Serikali inajipanga upya kuona ni namna gani Mgodi huo uendeshwe ili kuhakikisha unaleta tija kwa Taifa na siyo kuleta hasara kama ilivyo sasa.
Alisema kuwa, baada ya Serikali kubaini kuwa hasara iliyopatikana katika Mgodi huo imesababishwa na Mgodi kutosimamiwa vizuri, ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwasimamisha kazi wahusika pamoja na kutuma Timu kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwenda kuhakiki madeni husika.
“Kwa hivyo, tumeamua kusimamisha shughuli zote pale, tujihakikishie yale madeni. Uchunguzi unaendelea na baada ya muda tutatoa msimamo wa Serikali kuhusu namna bora ya kuuendesha ule Mgodi.”
Baada ya kukutana na kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Uslama ya Mkoa, Naibu Waziri pia alitembelea Ofisi za Madini za Mkoa na kuzungumza na wafanyakazi.
Naibu Waziri anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ambapo akiwa mkoani Kagera, anatarajiwa kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa Madini ya Bati, kukagua maendeleo ya ujenzi wa Viwanda vidogo vya uongezaji thamani Madini hayo pamoja na kukagua Mradi wa Kabanga Nickel.
Imeandaliwa na:
Veronica Simba, Geita
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
Kikuyu Avenue,
P.O Box 422,
40474 Dodoma,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
BaruaPepe: info@mem.go.tz,
Tovuti: mem.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.