[Latest Updates]: Biteko Azitaka Taasisi za Madini Kufikiri Kibiashara

Tarehe : March 23, 2019, 2:50 p.m.
left

Waziri wa Madini Doto Biteko amezitaka taasisi zilicho chini ya Wizara kufikiri kibiashara ikiwemo kutafuta njia zitakazowezesha sekta ya madini kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Waziri Biteko ameyasema hayo Machi 23, jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kupitia na kujadili Mpango Mkakati na Mkakati wa Kibiashara wa Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) iliyoandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Aidha, amezitaka taasisi hizo kuhama katika mtindo wa kutegemea ruzuku ya serikali badala yake zijiendeshe kibiashara na kuwataka watendaji wa wizara na taasisi kuhakikisha wanafanya mageuzi yatakayowezesha sekta hiyo kuchangia zaidi sambamba na kasi yake ya ukuaji kiuchumi.

 “ Serikali kwa upande wake imeshafanya mageuzi makubwa. Tunataka Idara, kitengo na taasisi zifanye mageuzi. Tuwe na taasisi ambayo mfanyakazi anaweza kueleza amefanya nini kipya,” amesisitiza Waziri Biteko.

Pia, ameongeza kuwa, ukataji madini ni suala ambalo linalopaswa kuchukuliwa kwa uzito wa kipekee kutokana na umuhimu wake katika biashara ya madini na hususan kipindi hiki ambacho serikali inasisitiza shughuli za uongezaji thamani madini kufanyika nchini ikiwemo kuhamasisha ujenzi wa viwanda hivyo.

Vilevile, amewataka washiriki wa kikao hicho kuwasilisha mawazo chanya yatakayosaidia kuboresha mkakati huo utakopelekea uboreshaji wa kituo cha TGC.

Aidha, amewataka watendaji wa Kituo cha TGC kuhakikisha wanakitangaza kituo hicho ikiwemo kuwafanya wachimbaji wadogo wa madini kuwa marafiki wa kituo hicho.

Kwa upande wake, Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, amesema serikali iliona umuhimu wa Kituo cha TGC hali ambayo imepelekea kuandaliwa kwa mikakati hiyo na kueleza kuwa uwepo wake unapaswa kutoa mabadiliko katika kituo hicho na hususan katika eneo la uongezaji thamani madini.

 Ameongeza kuwa, uongezaji thamani madini ni jambo ambalo serikali inaliangalia kwa umuhimu wake na kueleza kuwa ni miongoni mwa mambo  yaliyopelekea kufanyika kwa mabadiliko katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na 2017 ili taifa liweze kunufaika zaidi .

Ameeleza masuala mengine yaliyopelekea serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya madini ni pamoja na kutaka kuongeza mapato ya serikali yanayotokana na madini, serikali kushiriki katika uchumi wa madini na kumiliki hisa, kushirikisha jamii katika miradi ya madini na kampuni za madini kushirikiana  na jamii.

Aidha, amewashukuru wataalam washauri Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutokana na ushauri wao walioutoa kwa wizara wakati wa kupitia Mikakati hiyo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara yaMadini, Prof. Simon Msanjila amewataka watendaji wa Wizara kuhakikisha kila mmoja anaangalia eneo linalomhusu katika kituo hicho na kulifanyia kazi kikamilifu ili kufikia lengo linalotarajiwa .

Wizara ya Madini iliona umuhimu wa kukiimarisha Kituo cha TGC ili kijiendeshe kibiashara kutokana na fursa zilizopo katika sekta ya madini hususan kwenye ukataji wa madini. Pia, kutokana na fursa zilizopo katika ukataji wa madini ya vito na jimolojia kwa ujumla, wizara iliona TGC inaweza kujiendesha kibiashara na hivyo kuongeza mapato kwa serikali.

Kazi ya kuandaa Mikakati hiyo imetekelezwa kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) na  kuandaliwa na Wataalam Elekezi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe na kupitiwa kikamilifu na Prof. Beatus Kundi na Prof. Marcellina Chijoriga kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizarani na taasisi zake.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals