[Latest Updates]: STAMICO Wajipanga Kuwafikia Wachimbaji Wadogo Nchi Nzima

Tarehe : April 9, 2023, 12:13 p.m.
left

Dkt. Mwasse awataka Wadau kusukuma Ajenda ya Viwanda kupitia Sekta ya Madini

DACOREMA Watoa Wito Wadau Madini ya Viwandani kushiriki mkutano kujadili changamoto*

CTI Yasisitiza Viwanda kutumia Malighafi za Ndani

TAWOMA Yasifu Mabadiliko ya STAMICO kama Mlezi wa Wachimbaji Wadogo

Asteria Muhozya na Bibiana Ndumbaro – Dar esSalaam

Katika kuhakikisha Tanzania inanufaika na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda Duniani  kupitia Sekta ya Madini, Shirika la Madini  la Taifa  (STAMICO)  limeazimia kuwafikia Wachimbaji  Wadogo wa Madini nchi nzima  ili  kutatua changamoto zinazowakabili  ikiwemo masoko, kupatiwa elimu kwa lengo la kuongeza kiwango cha uzalishaji wa madini wanayoyazalisha.

Hayo yamebainishwa Aprili 4, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse wakati akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar esSalaam ikiwa ni maandalizi ya kufanyika kwa mkutano wa Wachimbaji Wadogo na Wadau wa Madini ya Viwandani Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani utakaofanyika tarahe 5 na 6 jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko.

Akifafanua kuhusu mkutano huo, Dkt. Mwasse amesema, umeandaliwa na STAMICO kwa kushirikiana na Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani (DACOREMA) pamoja na Shirikisho la wenye viwanda ambapo pamoja na mambo mengine unalenga  kujadili na kuweka mapendekezo ya utatuzi wa changamoto zinazokabili uchimbaji na biashara ya madini ya viwandani hususan masoko, mitaji na zana za uchimbaji.

‘Tumenunua mashine za uchorongaji kupata sampuli. Sekta za uzalishaji zimepewa kipaumblele na sisi tunataka Sekta ndogo ya uchimbaji iunge mkono na inufaike zaidi,’’ amesisitiza Dkr. Mwasse.

Ameongeza kwamba, mkutano huo unatarajia kuwakutanisha wachimbaji wadogo, wamiliki wa viwanda ambao ni watumiaji wa madini ya viwandani, taasisi za fedha, wasambazaji vifaa na wasimamizi sheria,  wasimamizi wa kodi  na hivyo kutumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wa madini kujitokeza kushiriki mkutano huo ili kuwezesha kusukuma mbele ajenda ya  viwanda kupitia Sekta ya madini.

Pamoja na majukumu iliyopewa STAMICO kwa mujibu wa Sheria ya The State Mining Corporation (Establishemnt) Order 1972 na kuuhishwa mwaka 2015 (The State Mining Corporation, Establishment Order, 2015) inalo jukumu la kuratibu shughuli za uendelezaji wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwawezesha kupata taarifa za masoko, mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu kutoka taasisi za fedha pamoja na kuwawezesha kupata teknolojia za kisasa kwa ajili ya kufanya shughuli zao za uchimbaji. Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani (DACOREMA) Josephat Mkombachepa ametoa wito kwa wachimbaji wadogo kushiriki mkutano ambao mijadala yake mbali na kutatua changamoto zinazowakabili, pia, utawezesha kufikiwa kwa asilimia 10 ya mchango wa sekta ya  madini katika PatolaTaifa ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) Leodegar Tenga amewataka wanachama wa umoja huo kutumia malighafi zinazozalishwa nchini ili kutimiza vema wajibu wao kama watanzania kuhakikisha rasillimali madini zinasaidia kujenga uchumi wa viwanda nchini.

Aidha, Tenga ametaka viwanda vya ndani kufanya kazi kwa ufanisi huku vikizalisha bidhaa zenye ubora kwa ajili ya kushindana katika masoko ya kimataifa. Kufuatia hali hiyo, amewasisitiza wadau wa madini ya viwandani kushiriki katika mkutano huo ili kuweza kujadili masuala yanayogusa sekta hiyo ndogo na hatimaye isaidie katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi nchini.

‘’ Mkutano huu unalenga kuona tunasaidia vipi sekta hii ndogo, hatutaki kuwanufaisha wakubwa tu bali tunataka ajira kwa walio wengi na ushirikishi,’’ amesema Tenga.

Naye, Katibu wa Chama Cha Wanawake Wachimbaji Madini Tanzania (TAWOMA) Salma Ernest, ameipongeza STAMICO kwa kuchukua hatua inayowakutanisha wadau mbalimbali kujadili eneo hilo na kuitaka STAMICO kufanya mwendelezo wa kuwa na mikutano kama hiyo.

‘’ Kwetu sisi TAWOMA tukiona historia ya STAMICO tangu 2015 tunaona kuna mabadiliko makubwa yametokea, mkutano huu kwetu kama wachimbaji wanawake unatugusa kutokana na changamoto zinazotugusa zikiwemo masoko; ni mkutano ambao utatuunganisha,’’amesema Salma.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals