[Latest Updates]: Serikali yatoa Maamuzi Mgogoro wa Mita 23 Mgodi wa Irasamilo

Tarehe : Feb. 13, 2020, 9:16 a.m.
left

Waziri wa Madini, Doto Biteko amewataka Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini kutumia Ofisi za Wizara katika kufikisha changamoto zao badala ya kufikisha kero zao kwa viongozi wengine wa nchi na serikali wasio na dhamana ya kusimamia Sekta ya Madini,  kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha utatuzi wa kero zinazowakabili.

Waziri Biteko aliyasema hayo jana tarehe 12 Februari 2020, wakati wa kikao kilicholenga kumaliza mgogoro baina ya wachimbaji wadogo Magere Mang’era na Joseph Ocheng Ndugu waliokuwa wakigombea umiliki wa eneo la mita 23 lililopo katika leseni  ya Irasamilo Gold Mine iliyopo Buhemba Wilaya Butiama mkoani Mara.

Pamoja na hayo, Waziri Biteko aliwataka wachimbaji wa Mkoa wa Mara kupunguza migogoro na kuwaeleza wizara yake  inatamani kukutana nao kwa nia njema na si kwa lengo la kujadili na kutatua migogoro ambayo inarudisha nyuma maendeleo yao na nchi kwa ujumla.

“Wizara inashughulika na sekta ya madini nchi nzima, kama kila mchimbaji atataka kuleta malalamiko yake ofisini kwa waziri basi kazi hazitafanyika.” Tungefurahi kukutana nanyi kuwaeleza vitu mnavyotakiwa kuviboresha ili kuongeza mapato ni si kutatua migogoro, Biteko alisisitiza.

Aidha, Biteko ameutaka uongozi wa mgodi na uongozi wa wachimbaji wadogo ngazi za wilaya na mkoa (Marema) kuhakikisha kwamba amani inatawala kwa wachimbaji na kuwafanya wachimbaji wachimbe na kuzalisha kuliko kutengeneza migogoro isiyoisha inayochangia katika kurudisha nyuma maendeleo yao. “Wanaotafuta pesa hawatumii muda mwingi kugombana”, amesisitiza Biteko.

Baada ya kufikia hatma ya mgogoro huo na kumtaka Afisa Madini Mkazi Nyaisara Mgaya kusimamia haki katika eneo hilo kama kikao kilivyoafiki kuwa mwenye haki ya kupewa eneo hilo ni Magere Mang’era, Biteko aliwataka wajumbe walioshiriki kikao hicho kurudi Mara na kuendelea na shughuli za uzalishaji huku wakitunza amani na ushirikiano miongoni mwao.

Aidha, aliwataka kumtumia Afisa Madini Mkazi aliyepo katika eneo hilo kama mlezi lakini pia alimtaka Afisa huyo kuishi na wachimbaji hao vizuri na kudumisha ushirikiano wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo aliutaka uongozi wa Wachimbaji wadogo wa madini (Marema) kusimamia haki kwa wananchi waliowapa dhamana ya kuwaongoza ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara  kwa mara.

"Mkoa wa Mara umejaliwa kuwa na rasilimali madini nyingi, msigeuze neema hiyo kuwa chanzo cha migogoro na kutishiana maisha",  alisema Naibu Waziri Nyongo.

Aliendelea kusema  Neema ya Rasilimali madini inapogeuka na kuwa  chanzo cha matatizo na migogoro inahuzunisha.

Aidha, Nyongo alizitaka pande zote kukubaliana na matokeo na kuwa maamuzi yaliyofikiwa yasiwe chanzo cha mgogoro mwingine, "naomba kabisa amani itawale".

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuheshimu maamuzi ya Serikali  na kutokuifanya serikali kutumia gharama kubwa katika kutatua migogoro ya wachimbaji badala yake muda unaotumika kutatua migogoro utumike kukusanya mapato ya serikali.

“Tumeweka ofisi za madini mikoani ili kupunguza matatizo madogo madogo kuletwa wizarani hivyo mzitumie ofisi hizo na kuamini maamuzi yanayotolewa na viongozi katika mikoa yenu yanakuwa  Baraka zetu”. Msanjila alisisitiza.

Prof. Msanjila aliwahakikishia wajumbe kuwa maamuzi yaliyofikiwa na Wizara ni sahihi na ya mwisho na kubainisha kuwa endapo hawakubaliani na maamuzi hayo basi wasingefika katika kikao hicho.

Profesa Msanjila alisisitiza kuwa, mlango sahihi wa kutatua migogoro katika sekta ya madini ni Wizara ya Madini vinginevyo ni kupoteza muda na rasilimali.

Kwa upande wa wajumbe walioshiriki kikao hicho wengi walikiri kuwa mwenye haki ya kupewa eneo lililokuwa na mgogoro ni Magere Mang’era na kwa Mamlaka aliyonayo Waziri aliamuru eneo lenye mgogoro apewe mlalamikaji na kuhitimisha mjadala juu ya mgogoro huo

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals