Tarehe : Jan. 4, 2019, 10:25 a.m.
Na Nuru Mwasampeta
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wa madini kuwa wazalendo na waaminifu kwa nchi kwa kulipa kodi stahiki zinazotokana na biashara ya madini wanayoifanya.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Umma. Pamoja na wachimbaji wadogo wa madini waliohudhuria mafunzo yanayotolewa na wizara ili kuboresha utendaji wao.[/caption]
Biteko amesema anashangazwa kuona kuwa mchango wa wachimbaji wadogo katika pato la taifa ni mdogo ilihali asilimia 96 ya shughuli za uchimbaji zinafanywa na wachimbaji wadogo na asilimia nne tu zimeshikwa na wachimbaji wakubwa na ndio wanachangia Zaidi katika ukuaji wa pato la taifa.
Biteko amebainisha kuwa hayo ni matokeo ya ukwepaji wa baadhi ya wachimbaji wadogo katika kulipa kodi stahiki zitokanazo na uchimbaji wa madini.
Ameyasema hayo leo tarehe 2 Januari, 2019 wakati akifungua rasmi mafunzo kwa wachimbaji wadogo katika eneo la Katente mkoani Geita.
Akifungua mafunzo hayo, Biteko amesema, mnamo mwaka 2016 Serikali ilitenga kiasi cha dola za kimarekani 3,703,630 kwa ajili ya utafiti wa kina wa jiosayansi chini ya mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP) ili kuboresha maisha ya mchimbaji mdogo na kutatua changamoto zinazomkabili ikiwa ni pamoja na uzalishaji mdogo na uchimbaji usiozingatia usalama na afya kwa mchimbaji.
Biteko alibainisha kuwa kazi ya utafiti katika mji wa Katente umekamilika kama inavyoshuhudiwa kupitia mafunzo yanayotolewa kwa wachimbaji wadogo wa eneo hilo yatakayosaidia kupunguza upotevu wa muda, uharibifu wa mazingira, upotevu wa mitaji pamoja na upotevu wa madini ya dhahabu yanayotokana na uelewa wa namna ya kufanya kazi hiyo.
Aidha, Biteko alibainisha kuwa, Baada ya matokeo ya utafiti huo uliofanywa kwa ushirika baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) na kubaini changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo katika kukua kiuchumi.
Wachimbaji wadogo wa madini katika mji wa Katente wakifuatilia kwa makini mafunzo juu ya uchimbaji wa madini yanayoendelea kutolewa na Wizara ya Madini[/caption]
Kutokana na changamoto zilizobainishwa na utafiti huo, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanza kujenga madarasa na kufunga mitambo kwa ajili ya mafunzo Zaidi na kubainisha kuwa eneo la Katente ni moja kati ya maeneo ambayo mafunzo hayo yatatolewa.
Pamoja na kupewa mafunzo hayo, Biteko amewataka wachimbaji hao kuunda vikundi na kufanya shughuli zao ndani ya vikundi ili kuirahisishia Serikali kuwatambua na kuwapa huduma stahiki zitakazowawezesha kuboresha kazi zao pamoja na afya zao.
Akizungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya uchimbaji mdogo; Biteko alisema ni pamoja na kuendelea kutenga maeneo maalaum kwa ajili ya wachimbaji wadogo, kutoa ruzuku, kurahisisha utoaji wa leseni, pamoja na kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwapa wachimbaji wadogo uelewa katika shughuli ya uchimbaji.
Utafiti huo ulifanyika kufuatia nia na adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais Dr. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha kuwa wachimbaji wadogo wanaondokana na uchimbaji usio na tija na kwenda kwenye uchimbaji utakaoongeza kiasi cha uzalishaji na baadaye kuongeza kipato kwa wachimbaji wadogo na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Jioloji kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Maruvuko Msechu alisema mafunzo yanayofunguliwa ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye lengo la kuhakikisha watanzania wanafaidika na uwepo wa madini nchini ili kujiondoa katika lundo la umaskini kwa kuongeza kipato na kuimarisha sekta mtambuka za uchumi.
Msechu alisema, Utafiti huo ulifanyika katika maeneo ya Ngazo, Kereza, na Katente wilayani Bukombe ukihusisha matumizi ya taaluma ya jiolojia, jiofizikia, na jiokemia ukihusisha uchukuaji wa sampuli mbalimbali za udongo na miamba.
Msechu aliongeza kwa kusema kuwa matokeo ya utafiti huo yalipelekea kufanyika kwa utafiti wa kina katika eneo la Katente, utafiti ulioanza rasmi tarehe 28 mwezi Oktoba, 2016 ambao ulipelekea jumla ya chorongo 19 za DD na 24 za RC kuchorongwa na kukusanya jumla ya sampuli 2821.
Aidha aliushukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Mkuu wa Wilaya pamoja na kamati ya ulinzi ya wilaya ya Bukombe kwa ushirikiano waliouonesha kipindi chote cha kufanya utafiti huo.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.