[Latest Updates]: Nyongo asuluhisha mgogoro wa wachimbaji madini Ishokelahela

Tarehe : April 28, 2018, 12:24 p.m.
left

  • Kamishna Msaidizi Kanda ya Ziwa atoa maagizo mwekezaji alipe fidia

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amefanikiwa kusuluhisha mgogoro baina ya wachimbaji madini wadogo wa vikundi vya Basimbi na Buhunda vilivyopo eneo la Ishokelahela, wilayani Misungwi, Mkoa wa Mwanza ambao umedumu kwa miaka Saba.

Sehemu ya Mgodi wa Dhahabu wa Isinka uliopo eneo la Ishokelahela wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, kama ulivyoonekana wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), jana Februari 22, 2018.[/caption]

Akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kazi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, Naibu Waziri Nyongo alikutana na viongozi na baadhi ya wanavikundi vya wachimbaji hao, katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda na kuendesha kikao cha usuluhishi huo.

Akitoa maamuzi ya usuluhishi, baada ya kuzungumza nao, Naibu Waziri aliwataka wachimbaji hao, ambao kimsingi hawana leseni na wamevamia eneo la mwekezaji Carlton Kitongo, kuachana na malumbano na waungane pamoja ili waendelee na shughuli za uchimbaji katika eneo ambalo mwekezaji huyo ameamua kuwapatia.

“Mwekezaji amekubali kuwaachia eneo ili muungane na kuchimba kwa pamoja. Hivyo ninawataka make pamoja muelewane na muendelee na shughuli za uchimbaji katika eneo mlilopewa.”

Hata hivyo, Naibu Waziri alibainisha kuwa, eneo ambalo moja ya vikundi hivyo walivamia na hawataki kuliachia, haliruhusiwi kufanya shughuli yoyote ikiwemo uchimbaji, kwa mujibu wa Sheria ya Madini, kwa kuwa ni eneo lililotengwa kwa taratibu za kiusalama (buffer area) kutokana na shughuli za ulipuaji miamba kwa baruti na nyinginezo zinazofanyika Mgodini.

“Kwa sababu hiyo, haiwezekani ninyi kuendelea kuchimba katika eneo hilo kwani sheria hairuhusu,” alisisitiza Naibu Waziri.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji hao na wengine kote nchini, ambao wanachimba madini pasipo kuwa na leseni halali zinazotolewa na Serikali, kuhakikisha wanafanya utaratibu wa kuomba ili wapatiwe leseni na hivyo watambuliwe na Serikali na kuweza kufanya kazi zao kwa Amani.

Sehemu ya umati wa wananchi wa Ishokelahela wakiwa katika ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), jana Februari 22, 2018.[/caption]

Alisema kuwa, lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuilinda Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ambayo inaelekeza watu wachimbe madini kwa tija ili waongeze kipato chao na kuchangia katika uchumi wa nchi kwa kulipa kodi na tozo nyingine stahiki.

Vilevile, aliwataka wachimbaji madini kote nchini kuendesha shughuli zao kwa kufuata Katiba zao walizojiwekea, bali muhimu zaidi kufuata sheria ya madini na kanuni zake mbalimbali zinavyoelekeza.

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, akiunga mkono maagizo ya Naibu Waziri Nyongo, alisema kuwa umefika wakati kwa wachimbaji wote wa madini kuhakikisha wanakuwa na nakala ya Sheria ya Madini, waisome muda wote na kujikumbusha kuhusu wajibu na haki zao.

Aidha, aliwataka wachimbaji wadogo wenye tabia ya kuvamia maeneo yenye leseni za wawekezaji kuacha mara moja bali wabaki katika maeneo yao na kuendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Mbunge wa Misungwi Charles Kitwanga, pamoja na kuafiki maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri, aliwataka wachimbaji hao kujenga tabia ya kuheshimu mikataba yao ya kazi ili waweze kufanya kazi katika mazingira yenye amani hivyo kuepuka migogoro.

Shimo wanalochimba dhahabu wachimbaji wadogo wa Kikundi cha Basimbi kilichopo eneo la Ishokelahela wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza. Hapa ni wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo jana, Februari 22, 2018.[/caption]

Akizungumza katika kikao hicho, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina aliwataka wachimbaji wenzake kote nchini kuwa na umoja na kujenga tabia ya kuwajibika.

Awali, akieleza namna Serikali inavyowajibika katika kutetea na kusimamia haki za wachimbaji wadogo, Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahya Samamba alibainisha kuwa hakuna mwekezaji yeyote anayeruhusiwa kufanya shughuli za uchimbaji kabla ya kuwalipa fidia wananchi wenye maeneo ambayo yatakuwa ndani ya leseni yake.

Sambamba na ufafanuzi huo, Mhandisi Samamba alitoa maagizo kwa mwekezaji wa Mgodi wa Isinka, kuhakikisha anamlipa mwananchi mwenye eneo ambalo liko ndani ya leseni yake, Mama Malosha Lutamla kabla ya kuanza kazi kwa Mgodi huo.

Naibu Waziri Nyongo anaendelea na ziara yake katika Mikoa mingine ya Kanda ya Ziwa, ambayo ni pamoja na Geita, Kagera na Kigoma.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba, Mwanza

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: www.madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals