Tarehe : Aug. 13, 2018, 6:52 a.m.
Na Asteria Muhozya, Arusha
Waziri wa Madini Angellah Kairuki amewataka Wafanyabiashara wa Madini nchini kuzaliwa upya kwa kufuata Sheria, Kanuni na taratibu kwa kufanya biashara halali ya madini ili kuziwezesha pande zote yaani Serikali na Wafanyabishara kunufaika na rasilimali hiyo.
Sehemu ya wafanyabishara wa madini wa jijini Arusha wakifuatilia mkutano baina yao na Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani).[/caption]
Waziri Kairuki ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wafanyabiashara wa madini wa jijini Arusha waliohudhuria mkutano huo ulioratibiwa na Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania, (TAMIDA).
Kairuki alisema zama zimebadilika na hivyo kuwatahadharisha wale wote wanaofanya vitendo vilivyo kinyume na taratibu na kueleza kuwa, hawatasalimika na mkono wa sheria kwa kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba rasilimali madini inawanufaisha watanzania na taifa.
“Nimekuja hapa tubatizane. Naomba tuzaliwe upya. Tushirikiane vizuri. Naahidi kuwa balozi wenu mzuri. Nitatekeleza yale yenye manufaa kwetu sote. Lakini watakaokwenda kinyume, serikali ina macho yanayoona sana na yenye lenzi za hatari,” alisisitiza Kairuki.
Kairuki alisisitiza kuwa, tayari anazo taarifa za kila mfanya biashara wa madini wa jijini Arusha na kuwataka wote wanaokwenda kinyume kujitafakari upya na kuchukua hatua sahihi kwani anamfahamu kila mmoja.
Alisema, serikali inatambua na kuthamini mchango wa biashara ya madini katika pato la taifa na katika kuzalisha ajira na kuongeza kuwa, itaendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara ya madini na kuwataka wale wote waliokuwa wakitenda kinyume ikiwemo kukwepa kodi kujisalimisha kwake ili kuepuka kuingia katika makosa ya uhujumu uchumi.
“Kama unadhani ulikuwa unakwepa kodi, unakwenda kinyume, njoo uniambie. Haitapendeza upate kosa la uhujumu uchumi, kumbukeni kuwa kosa hilo halina dhamana,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Akizungumzia suala la utoaji leseni za usafirishaji madini nje ya nchi, alisema serikali italifanyia haraka suala hilo ili kuleta ufanisi katika biashara ya madini huku akisisitia kuwa, watakaopatiwa leseni hizo ni wale tu watakaokidhi vigezo.
Mmoja wa wafanyabishara madini akimwonesha Waziri wa Madini Angellah Kairuki madini aina ya Ruby na kumweleza kuhusu ukubwa tofauti wa madini hayo na suala zima la uongezaji thamani madini hayo kabla ya kusafirishwa.[/caption]
Aidha, Waziri Kairuki alitumia fursa hiyo kukaribisha wawekezaji katika sekta ndogo ya Uongezaji thamani madini na kueleza kuwa, serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba shughuli za uongezaji madini zinafanyika nchini ikilenga kuongeza mchango wa madini katika pato la taifa na kuzalisha ajira.
Aliwataka wafanya biashara wa madini wenye nia kuwekeza katika viwanda vya ukataji na unga’rishaji madini ya vito kufanya hivyo na kuwasilisha mapendekezo serikalini ili kuna namna bora ya kufanikisha suala husika.
Kairuki aliongeza kuwa, masuala ya uongezaji thamani madini nchini ni moja ya mapendekezo katika Sheria mpya ya madini na kuelea kuwa, mwongozo wa namna ya shughuli za uongezaji thamani madini zitakavyofanyika utatolewa na serikali baada ya kukamilisha suala hilo.
“ Lakini pia hatukatazi wageni kuwekeza nchini. Isipokuwa tunataka waje kihalali,” alisisitiza Waziri Kairuki.
Awali, akisoma risala ya wafanyabiashara hao, Mwenyekiti wa TAMIDA Sam Mollel, alisema, TAMIDA inaunga mkono suala la uongezaji thamani madini kufanyika nchini kwa kuwa shughuli hizo zitasaidia kuongeza thamani ya madini, fedha za kigeni kuhamisha teknolojia, kupanua wigo wa ajira na kufungua viwanda vingi vya uongezaji thamani na hatimaye kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha madini barani Afrika.
Vilevile, alisema kuwa, chama hicho kinaunga mkono kutosafirisha madini ghafi ya Tanzanite nje ya nchi na kupendekeza kuwa madini ya tanzanite yanayozidi gramu 1 yakatwe hapa nchini na kwa yale yaliyo nusu uzito yaongezwe umbile kisha yaruhusishwe kusafirishwa yakiwa ghafi kwa kuwa bado hakuna ujuzi wa kukata madini katika kiwango hicho.
“Mhe. Waziri tunapendekeza mchakato huo ufanyike hivyo wakati tukiendelea na kupata ujuzi na wataalam katika suala hilo na baada ya muda basi liwekwe zuio,” alisema Mollel.
Sehemu ya wafanyabishara wa madini wa jijini Arusha wakifuatilia mkutano baina yao na Waziri wa Madini Angellah Kairuki (hayupo pichani).[/caption]
Pia, alisema Tamida inapendekeza Kamati Pamoja ya kupanga bei elekezi za madini huku ikishirikisha serikali na wadau wa madini na pia kuiomba serikali kuangalia mifumo ya kodi.
Akizungumzia ujenzi wa ukuta unaozunguka migodi ya tanzanite Mirerani, alisema kuwa, Tamida inaunga mkono jitihada zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli na kueleza kuwa, ukuta huo umesaidia kulinda rasilimali na udhibiti wa madini hayo.
Mollel aliongeza kuwa, ukuta wa mirerani umezuia uingiaji holela katika migodi hiyo kwa kuwa kila mwingiaji inampasa kuwa na kitambulisho na uwepo wa geti moja tu.
Pia, alisema kuwa, ukuta huo umeongeza Imani kubwa kwa walaji wa madini hayo zikiwemo nchi za Marekani na Ulaya na kuongeza kuwa, “ukuta umedhibiti ajira za watoto migodini na kuondoa wizi wa vifaa migodini”.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.