[Latest Updates]: Taarifa Sahihi za Kijiolojia Ndiyo Utajiri wa Watanzania - Waziri Mavunde

Tarehe : Nov. 10, 2023, 7:39 p.m.
left

TAARIFA SAHIHI ZA KIJIOLOJIA NDIYO UTAJIRI WA WATANZANIA – WAZIRI MAVUNDE.

#Asema kupitia taarifa hizo Sekta ya Madini itafungamanisha sekta nyingine

#Asisitiza itamaliza migogoro ya Wachimbaji Wakubwa na Wadogo

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amesema kuwa uwepo wa taarifa sahihi za kijiolojia za miamba ndiyo zimebeba dhana ya utajiri na maisha bora kwa Watanzania.

Amesema hayo leo Novemba 10, 2023, jijini Dodoma, wakati akizungumza katika kipindi cha runinga na radio cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi Media.

Amesema kuwa dhana ya Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri ni kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali madini kwa kutengeneza matajiri wengi kupitia Sekta ya Madini sambamba na kuboresha maisha ya Watanzania na kwamba hayo ni maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona madini yanaleta maisha bora kwa Watanzania.

Waziri Mavunde amesema ili kutimiza malengo hayo, Serikali imekuja na mkakati wa kuiongezea uwezo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili ifanye utafiti wa kina wa miamba yote yenye madini iliyopo hapa nchini kwa lengo la kutengeneza kanzidata ya taarifa sahihi za kijiolojia.

“Malengo yetu ni kufanya tafiti za kina kwa angalau asilimia 50 kufikia asilimia 2030, ukilinganisha na sasa ambako ni asilimia 16 pekee ndiyo imefanyiwa utafiti wa kina kwa kutumia teknolojia ya kisasa, unaweza kuona mchango mkubwa iliyonao sekta ya madini pamoja udogo wa sehemu iliyofanyiwa utafiti wa kina wa miamba, sasa tukifanya mara tatu ya hapo tutakuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi sambamba Pato la Taifa kwa ujumla” amesema Mhe. Mavunde

Aidha, amesema kuwa taarifa hizo zitaenda kufungamanisha Sekta ya Madini na sekta zingine zikiwemo za Kilimo, Maji,  Afya sambamba na uchumi kwa ujumla.

“Tukizungumzia maisha, tafiti hizi zitatuonesha sehemu maji yalipo, maji safi na salama ni muhimu kwa maisha ya watu wetu, lakini pia Wizara ya Kilimo ina mkakati wa kujenga mabwawa 100 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kuacha kutegemea mvua zisizotabirika pia madini ya jasi yanasaidia kuondoa tindikali kwenye ardhi kwa ajili ya kilimo, mpaka hapo unaweza kuona jinsi sekta ya madini inavyogusa maisha wa Watanzania kupitia kilimo na maji.” amesema Mhe. Mavunde.

Amesema taarifa za tafiti hizo pia zitafungamanisha Sekta ya Afya kwa kuwa zitasaidia kujua miamba yenye gesi ya Hellium ambayo inatumika katika teknolojia ya upigaji picha za kina za anatomia (MRI), vipimo vinavyotumika hospitalini, na hivyo kuonesha jinsi sekta ya madini inavyoenda kugusa sekta ya afya.

Sambamba na hilo, Waziri Mavunde amesema kuwa uwepo wa taarifa hizo zitasaidia kuondoa  migogoro baina ya wachimbaji wakubwa na wadogo kwasababu chanzo cha migogoro hiyo ni wachimbaji wadogo kuamini madini yapo kwenye maeneo ya wachimbaji wakubwa kwa kuwa yamefanyiwa utafiti wa kina, hivyo migogoro hiyo itaisha baada ya kupata maeneo mengine yaliyofanyiwa tafiti .

“Tunataka Wachimbaji wadogo waache kuchimba kwa kubahatisha, madini sio ushirikina wala bahati ni sayansi, wachimbe kwa kuwa na uhakika kutokana na taarifa sahihi za kijiolojia, kwa kufanya hivi tutaokoa mitaji yao kwa kuwa watachimba kwa uhakika na kuuza madini wanayopata, watalipa mikopo waliyonayo, lakini pia watapata mikopo kwa kuwasilisha taarifa hizi kama dhamana katika taasisi za kifedha tofauti na sasa ambako wanalazimika kuweka dhamana nyumba, viwanja na mali zao zingine.” ameongeza Mhe. Mavunde.

Waziri Mavunde amehitimisha wiki ya Vision 2030, Madini ni Maisha na Utajiri ambapo Wizaya ya Madini na Taasisi zake zilipata fursa ya kuelezea mikakati na utekelezaji wa dira hiyo kufikia mwaka 2030.

VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals