[Latest Updates]: Doto Biteko atoa maagizo mazito kwa wachimbaji kokoto Dodoma

Tarehe : Dec. 31, 2018, 10:21 a.m.
left

Na Nuru Mwasampeta

Kufuatia ziara ya Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa  aliyoifanya hivi karibuni katika eneo la Ihumwa ambako ujenzi wa Mji wa Serikali unaendelea  na kubaini uhaba wa kokoto katika ujenzi huo,  leo Disemba 30, Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko akifuatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Ajira na Vijana Anthony Mavunde wamefanya ziara ya kushtukiza kwenye maeneo yanayochimba kokoto hizo na kubaini madudu.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, akitoa tamko la Serikali kwa wachimbaji wa kokoto alipofanya ziara kujionea kinachoendelea katika machimbo hayo baada ya kubainika uhaba wa kokoto katika eneo la ujenzi wa ofisi za Serikali Ihumwa jijini Dodoma.[/caption]

Naibu Mawaziri hao wamebaini machimbo ya kokoto yakiwa yamefungwa kwa madai kuwa wafanyakazi wako likizo, zikiwemo mashine za kusagia mawe hayo zikiwa  zimeharibika kwa takribani miezi mitatu na hivyo kupelekea uzalishaji kusimama.

Akizungumza katika eneo hilo la machimbo, Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema anashangazwa kuona kuwa watumishi katika mgodi wa kokoto wanakwenda likizo wakati mahitaji ya kokoto ni makubwa  na soko la  uhakika.

“Mmechukua  zabuni  kwa ajili ya kusambaza kokoto kutoka kwa   Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC),na  kampuni ya MZINGA wenye uhitaji mkubwa kwa ajili ya ujenzi wa mji wa Serikali unaoendelea halafu mnadai mko likizo,?” amehoji Biteko.

Akizungumza  kwa njia ya simu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Laroy Aggregate Co. Ltd , Biteko amemtaka  mkurugenzi huyo aliyefahamika kwa jina la Joel Mchovu kuhakikisha kuwa, ifikapo  Januari 2, 2019 kokoto ziwe zimezalishwa na kusambazwa kwa wahitaji kama walivyokubaliana ili ujenzi uendelee kwa kasi iliyokusudiwa.

Aidha, amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa juhudi na weledi mkubwa ili kuzalisha kiasi kinachotosheleza mahitaji vinginevyo oda zitahamishwa na kupewa kampuni za zinazozalisha kokoto zilizopo Chalinze ambazo zinaonesha  uwezo mkubwa katika uzalishaji wa kokoto.

“Mfahamu kwamba endapo tutatoa oda kwa watu wa Chalinze maana halisi ya ujenzi wa mji wa Serikali kwa watu wa Dodoma haitakuwepo kwani hamtanufaika na ujenzi huu,” amesisitiza Biteko.

Biteko amewataka wananchi wa Dodoma kutambua kuwa, ujenzi wa mji wa Dodoma ni fursa kwao ya kuweza kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao binafsi hivyo, wanapaswa kuwajibika ili kupata manufaa hayo. “Fursa kubwa imepatikana na soko la uhakika lipo nitawashangaa kuona kuwa mnapoteza fursa hii,” amesisitiza.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akisaini kitabu cha wageni alipotembelea katika machimbo ya kokoto ya kampuni ya Laroy Aggregate Co. Ltd, Kulia kwake ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthon Mavunde na kushoto ni msaidizi wake Kungulu K. Masakala[/caption]

Naye, Fundi wa Mitambo ya kuchoronga mawe katika mgodi wa WADI, Gao Peng, amesema kuwa, kampuni hiyo iko katika hatua za kutengeneza mashine iliyoharibika ili kuwawezesha kuendelea na uzalishaji wa kokoto hizo na kueleza kwamba mashine hiyo imeharibika kwa takribani kipindi cha  miezi mitatu sasa na hivyo kufanya uzalishaji wa kokoto hizo kusimama.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Vijana Anthony Mavunde, amesema anajisikia vibaya kuona kazi katika maeneo ya machimbo hazifanyiki na kuwataka wananchi wanaofanya shughuli hizo kuongeza nguvu, weledi na ufanisi ili  waweze kunufaika.

“Dodoma tumejaliwa kuwa na mawe mengi ya kuzalisha kokoto na madini mengine ya ujenzi, mahitaji ni makubwa kutokana na kasi ya ujenzi iliyopo lakini bado wana Dodoma mmelala,” amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Afisa Madini wa Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Jonas Mwano amekiri kuwepo kwa leseni hai za uchimbaji wa madini ya kokoto 75 katika mji wa Chigongwe na leseni 66 zimekwisha tolewa kwa waliowasilisha maombi ya leseni hizo na hivyo kuwataka wamiliki wa leseni hizo kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni zao vinginevyo zitagawiwa kwa watu wengine.

Aidha, Mwano amekiri kuwa, awali wamiliki wengi wa leseni za madini ya kokoto walikuwa hawazalishi vya kutosha kwa madai kuwa soko lilikuwa adimu lakini sasa soko ni la uhakika na hivyo kuwataka wazalishe kokoto za kutosha ili kutoiangusha Serikali.

Pia, Mhandisi Mwano ameahidi kutembelea maeneo ya uchimbaji wa kokoto kila siku kufuatia maagizo ya Naibu Waziri Doto Biteko ili kuhakikisha kazi ya uzalishaji wa kokoto hizo unaridhisha na kutosheleza mahitaji ya ujenzi katika jiji la Dodoma.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals