Tarehe : April 28, 2018, 2:40 p.m.
Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini vya Mikoa yote Nchini (REMAs) vimetakiwa kuwaelimisha Wachimbaji Wadogo umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati) akijadiliana jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga alipofanya ziara kwenye machimbo ya dhahabu ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi.[/caption]
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alitoa agizo hilo Februari 24, 2018 kwenye mkutano na Wachimbaji wa madini kwenye machimbo ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi.
Naibu waziri Biteko alikutana na wachimbaji wadogo kwenye machimbo hayo ambao walimueleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo ukosefu wa vifaa, elimu na maeneo ya uchimbaji.
Biteko aliwahakikishia wachimbaji madini kote nchini kuwa Serikali haina kikwazo nao na dhamira yake ni kuona wanakua na kufikia uchimbaji wa Kati ama hata Mkubwa.
“Rais John Magufuli anawajali sana wachimbaji wadogo, anataka kuona mnakua ili mpate manufaa zaidi kutokana na shughuli zenu hizi lakini pia jamii inayowazunguka na Taifa kwa ujumla linufaike kupitia nyinyi,”
Hata hivyo Biteko aliwataka wahakikishe wanatimiza wajibu wao wa kulipa kodi ambayo alisema ikilipwa kwa usahihi manufaa yake ni makubwa kwao wao kama wachimbaji lakini pia kwa jamii inayozunguka maeneo ya uchimbaji na Taifa kwa ujumla.
“REMAs waelimisheni wachimbaji kulipa kodi. Hatuwezi kuiendeleza Tanzania yetu kama mnakwepa kulipa kodi,” alisema Naibu Waziri Biteko.
Alibainisha kuwa rasilimali madini ni kwa ajili ya Watanzania wote na kwamba kila mwananchi anayo haki ya kunufaika nayo kwa namna mbalimbali ikiwemo kupitia kodi zinazolipwa kutokana na shughuli za uchimbaji.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto) akisalimiana na Wachimbaji wadogo kwenye machimbo ya Dhahabu ya Kapanda yaliyopo katika Kata ya Machimboni, Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi.[/caption]
“Mtakavyolipa kodi, fedha hiyo itatumika kuwaletea na kuwaboreshea huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya na miundombinu mbalimbali,” alisema Biteko.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuwarasimisha Wachimbaji wa Madini kwa kuwapatia Leseni za Uchimbaji ili wachimbe kwa kufuata utaratibu unaotakiwa kama inavyoelekezwa kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.
Alisema Sheria husika vilevile inazungumzia suala la uundaji wa Tume ya Madini yenye jukumu la kusimamia shughuli zote za madini ikiwemo utoaji wa leseni ambayo alisema itaanza kazi hivi karibuni.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali inao wajibu wa kuwaelimisha wachimbaji wadogo umuhimu wa kulipa kodi ili kuwa na uchimbaji wenye tija na aliagiza Halmashauri za Wilaya, Ofisi ya Madini na Vyama vya Wachimbaji Wadogo kote nchini kushirikiana kuelimisha wananchi wajibu wao wa kulipa kodi na umuhimu wake.
Biteko vilevile aliwahakikishia Wachimbaji hao kupatiwa maeneo ya kuchimba ambapo alibainisha kuwa leseni za maeneo yasiyoendelezwa zitafutwa na maeneo hayo kupewa wale wenye nia ya dhati ya kuyafanyia kazi.
Imeandaliwa na:
Mohamed Saif, Katavi
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.