[Latest Updates]: Wataalam Wachambua Jiolojia ya Tanzania, Nishati Mbadala

Tarehe : Oct. 6, 2022, 10:50 a.m.
left

Wataka uzalishaji wa umeme wa Makaa ya Mawe pia utumike

Wasisitiza umuhimu wa nishati ya jotoardhi

Wametaka tafiti zisiishie makabatini

Chuma ya Asanje-Dodoma yatajwa kwa ubora matumizi ya viwandani, tafiti zaidi zahitajika

Na Asteria Muhozya- Arusha

Wajiolojia nchini wameishauri Serikali kuweka kipaumbele katika matumizi ya nishati ya Jotoardhi na kuhimiza kuanza kutumia Makaa ya Mawe kuzalisha  nishati ya umeme  badala ya kutegemea chanzo cha gesi asilia.

Hayo yamebainishwa katika siku ya pili ya mkutano wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania (TGS) unaoendelea jijini Arusha ambao umeshirikisha wajiolojia wapatao 200 waliobobea katika nyanja mbalimbali.

Akizungumza katika mjadala baada ya kuwasilishwa kwa mada mbalimbali zilizogusia masuala ya nishati na madini, Mtaalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Meshack Kagya ametaka vita ya inayoendelea hivi sasa kati ya nchi za  Ukraine na Urusi  itumike kama funzo la kuhakikisha vyanzo mbadala vya nishati vinatumika na nchi inakuwa na umeme wa kutosha kupitia vyanzo hivyo kwa kuwa taifa linayo rasilimali za kutosha za kuzalisha nishati ya umeme.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya hiyo Prof. Abdulkarim Mruma amesema ni wakati sasa kama nchi kuanza kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme kutokana na uwepo wa hazina ya kutosha ya madini hayo lakini hadi sasa hakuna nishati yoyote inayozalishwa kupitia chanzo hicho.

Wakichangia hoja, wataalam wengi wameunga mkono kwa kuitaka Serikali kufanya maamuzi ya kutumia makaa ya mawe kuzalisha umeme ikichukuliwa kuwa, bado mataifa makubwa na yaliyoendelea yanaagiza na kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya viwandani kwenye nchi zao.

Aidha, wameshauri kutokana na unafuu wa nishati ya jotoardhi ikiwa ni pamoja na kukabiliana na   mabadiliko ya tabia nchi ambao ndio mwelekeo wa sasa wa maendeleo duniani hivyo, serikali inapaswa kuweka nguvu kubwa katika kuendeleza nishati ya jotoardhi kama chanzo kingine cha kuzalisha nishati ya umeme na kwa kuzingatia kuwa, tayari zipo tafiti kadhaa zimekwishafanyika.

Wamesema, kutegemea gesi pekee si salama kwa nchi kwa kuwa ni nishati ambayo inaweza kuisha ikizingatiwa kuwa, kwa sasa asilimia 62 ya nishati ya umeme inayozalishwa na kutumika nchini inatokana na gesi asilia pekee.

Akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa, mtaalam kutoka Wizara ya Nishati, Jacob Mayalla amesema Kampuni Tanzu ya Uendelezaji Jotoardhi (TGDC) iliyo chini ya Wizara ya Nishati inatarajia kuzalisha megawati 200 zinazotokana na chanzo hicho ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake, mtaalamu kutoka (TGDC) Adonias Mkangale amesema tayari kampuni hiyo imekwisha kuanisha maeneo matano ambayo yanaweza kuchorogwa mashimo ya utafutaji wa nishati hiyo na tayari Serikali imekwishakununua mtambo wa kuchoronga.

Awali ameeleza kuwa, kuchelewa kutekelezwa kwa mradi huo kulitokana na changamoto kadhaa ikiwemo gharama kubwa katika hatua za awali za utafiti, vifaa vya kisasa na fedha.

Awali, akiwasilisha mada katika mkutano huo, Madirisha Makungu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam ameeleza umuhimu wa nishati ya Jotoardhi kwa mustakabali na maendeleo ya nchi na kuielezea kuwa, kama nchi inaweza kuhamia katika matumizi ya nishati hiyo kutokana na unafuu wake, umuhimu wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Pia amesisitiza kuwa, nishati hiyo haina matokeo mabaya.

Naye, Doreen Nyahucho anayefanya kazi kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ametoa mada kuhusu andiko linalohusisha utafiti wa njia mbadala inayotumia mionzi ya sukuma umeme inayoweza kusaidia kugundua kanda zinazopenyeza nishati mvuke kwa urahisi katika hatua za awali za uzalishaji. Doreen ametoa ushauri kwamba, njia hizo zinaweza kutumiwa katika shughuli za tafiti ya nishati ya joto ardhi kwa hapa nchini.

Akiwasilisha mada katika mkutano huo, mtaalam kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa  Madini Tanzania (GST)  Yusto Joseph amependekeza wadau kufanya tafiti zaidi kwa ajili ya kuendeleza  madini ya chuma ya Asanje yanayopatikana mkoani Dodoma. Amesema kuwa, kutokana utafiti ulifanyika Asanje, chuma hiyo ina ubora na inafaa kwa matumizi mbalimbali ya viwandani.

Ameongeza kwamba, hivi sasa chuma hicho kinachimbwa na wachimbaji wadogo na wa kati na kununuliwa zaidi na viwanda vya saruji.

Katika siku ya kwanza baada ya ufunguzi wa mkutano huo, mada mbalimbali zilizohusu masuala yanayohusu sekta ya Madini ziliwasilishwa.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals