[Latest Updates]: Biteko atatua mgogoro sugu madini

Tarehe : Nov. 26, 2018, 9:07 a.m.
left

  • Ni baada ya kruhusu wananchi kijiji cha Mhandu kuendelea na  uchimbaji dhahabu

Na Greyson Mwase, Shinyanga

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameruhusu wananchi  wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga kuendelea na uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la utafiti wa madini hayo lililokuwa linamilikiwa na Menan Sanga kwa kushirikiana na kampuni ya  Lion Town.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.[/caption]

Biteko aliyasema hayo leo tarehe 24 Novemba, 2018 katika mkutano wa hadhara ulioshirikisha wananchi  wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa  huo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto za wachimbaji wa madini.

Katika ziara hiyo, Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, Mbunge wa Jimbo la Msalala, Ezekiel Maige, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Wataalam kutoka Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari.

Biteko alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini  haiwezi kuruhusu mwekezaji kumiliki eneo pasipo kuliendeleza, kutokulipa kodi inayohitajika Serikalini  huku wananchi wenye nia ya kuchimba katika eneo husika wakiendelea kuteseka.

Alisema kuwa, Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli imeweka mikakati mbalimbali ya uboreshaji wa Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja marekebisho ya Sheria ya Madini inayotambua madini kama rasilimali za watanzania wote.

“Madini ni mali ya watanzania wote, na sisi kama Serikali tumejipanga katika kuhakikisha kila mwananchi anashiriki kwa kiasi kikubwa katika umiliki wa rasilimali za madini, hivyo ninawaomba endeleeni kufanya kazi ya uchimbaji katika eneo hili wakati taratibu nyingine zikiwa zinaendelea,” alisema Biteko huku akishangiliwa na wananchi.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga kurasimisha wachimbaji wadogo wa madini waliopo katika eneo hilo pamoja na kuwapatia leseni za uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni za madini ili wawe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta ya madini.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kushoto) akipata maelezo jinsi shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu zinavyofanyika chini ya ardhi katika eneo la Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu.[/caption]

Pia alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga kuandaa orodha ya wachimbaji wote wa madini pamoja na taarifa za uzalishaji wa madini  yanayozalishwa na wachimbaji wa madini ikiwa  ni pamoja na kodi mbalimbali wanazolipa Serikalini.

Aliwataka wachimbaji wadogo hao kufuata sheria na kanuni za madini ikiwa ni pamoja na ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali zinazohitajika Serikalini na kusisitiza kuwa, Serikali haitasita kufuta leseni za madini pale watakapokiuka sheria na kanuni za madini.

Awali wakizungumza katika nyakati tofauti wananchi  wa kijiji cha Mhandu kilichopo katika Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga walisema kuwa awali eneo hilo lilikuwa likimilikwa kampuni ya Lion Town tangu mwaka 1989 kabla ya kukabidhiwa kwa Menan Sanga ambaye amekuwa  haendelezi uchimbaji katika eneo hilo  huku akiwafukuza wananchi ambao wamekuwa wakichimba madini ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji hao Innocent Deus alisema kuwa wachimbaji wadogo wa madini wanaochimba madini katika eneo hilo wamekuwa wakitishiwa maisha ikiwa ni pamoja na kupigwa mara kwa mara na walinzi waliowekwa na mmiliki wa eneo  hilo Menan Sanga

Deus alisema awali kikundi kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo kijulikanacho kwa jina la BMS kiliundwa na kuomba leseni ya uchimbaji wa madini katika Wizara ya Madini kupitia ofisi yake iliyopo mkoani Shinyanga lakini walishangaa kuambiwa kuwa leseni husika imeshaombwa na kutolewa kwa Menan Manga.

Aliomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuwapatia sehemu ya eneo hilo kwa ajili ya kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini huku taratibu nyingine zikiendelea ikiwa ni pamoja na urasimishaji na utoaji wa leseni ili waweze kuchangia kwenye pato la Taifa.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu uliopo katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani Shinyanga.[/caption]

Naye Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige mbali na kutoa pongezi kwa Naibu Waziri wa Madini kwa kutatua mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu aliiomba Wizara ya Madini  kuwapatia maeneo yenye  madini kwa ajili ya uchimbaji hususan katika eneo husika kwa kuwa madini ni tegemeo pekee kwenye uchumi wao.

Alisema kuwa, wananchi wengi wanaishi katika maisha magumu huku wakiwa na rasilimali za madini ya kutosha ambazo zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuwanufaisha na kuimarisha huduma nyingine za jamii kama vile miundombinu ya barabara, umeme na maji.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Biteko alifanya ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu ulioko katika eneo la Kakola Wilayani Kahama mkoani Shinyanga  lengo likiwa ni kuona shughuli za uchimbaji madini na kufuatilia  utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Madini, Angellah Kairuki tarehe 24 Aprili, mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Biteko aliutaka mgodi huo kuhakikisha unamaliza mgogoro kati yake na wananchi ikiwa ni pamoja na kutoa mchanga wa marudio ambao ni mali ya wananchi  wanaozunguka mgodi huo waliouacha wakati wakipisha shughuli za uchimbaji kwa mgodi huo kwa kufuata sheria na taratibu.

Aidha, aliutaka mgodi kuandika barua kwenda Tume ya Madini kwa ajili ya kuomba mwongozo  wa namna ya kutoa mchanga wa marudio na kuwakabidhi wananchi ambao ndio wamiliki wa awali wa mchanga huo wakati wakiendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo.

Aidha, Naibu Waziri Biteko  alikerwa na kitendo cha mgodi huo kutokulipa kodi ya mapato kwa takribani miaka 19 na kuendesha shughuli zake kwa kusuasua  kwa kisingizio cha kuwa mgodi umeamua kupunguza gharama za uendeshaji.

“Haiwezekani kama mgodi mnaamua kupunguza gharama za uzalishaji pasipo kushirikisha Serikali huku mkibadilisha umiliki wa leseni ya baruti wa kampuni nyingine na ni jambo ambalo halikubaliki kabisa,” alisisitiza Biteko.

Alielekeza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Sinyanga kuangalia iwapo kuna taratibu zimekiukwa ili taratibu za kisheria zichukuliwe.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals