Tarehe : Oct. 30, 2019, 7:38 a.m.
Na Greyson Mwase, Morogoro
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka wachimbaji wa madini ya ujenzi kuwa na mikataba ya utoaji wa huduma kwa jamii inayotambulika kisheria ili kuepuka migongano inayoweza kujitokeza baina yao na wananchi wa vijiji vinavyozunguka machimbo.
Profesa Kikula alitoa kauli yake katika nyakati tofauti mkoani Morogoro leo tarehe 30 Oktoba, 2019 kwenye ziara yake yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ujenzi pamoja na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wa madini hayo.
Katika ziara yake Profesa Kikula aliambatana na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Shija, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Morogoro (MOREMA), Dk. Omari Mzeru, Mwenyekiti wa Madini ya Ujenzi na Wachimbaji Wasio Rasmi, Aquilin Magalambula na Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Yahya Nania.
Wengine ni pamoja na Wawakilishi kutoka katika Kurugenzi ya Manispaa ya Morogoro, Kurugenzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Maafisa kutoka Tume ya Madini.
Profesa Kikula mara baada ya kusikiliza kero za wachimbaji wa madini ya ujenzi katika maeneo tofauti alielekeza kuwa ni vyema wachimbaji wa madini ya ujenzi wakahakikisha wanaingia makubaliano ya kisheria na wanavijiji wanaozunguka machimbo yao kuhusu utoaji wa huduma kwa jamii kama vile maji, barabara, ujenzi wa madarasa ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza mbeleni.
Katika hatua nyingine, Profesa Kikula aliwataka wamiliki wa machimbo ya mchanga kuhakikisha wanakuwa na mipango ya maandalizi ya ufungaji wa machimbo mara baada ya shughuli za uchimbaji kumalizika na kuanza kuitekeleza kwa kurudishia mashimo vizuri.
“Mnatakiwa kuwa na mpango wa kuanza kurudishia mazingira katika hali nzuri kabla ya shughuli za uchimbaji wa mchanga kuisha ili kuepuka mashimo ambayo ni hatari kwa wananchi,” alisisitiza Profesa Kikula.
Aidha, aliwataka wamiliki wa machimbo ya mchanga kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kazi kwa wafanyakazi hao kwa kuhakikisha wanakuwa na nyumba na vyoo salama ikiwa ni sehemu ya usalama kwenye machimbo hayo kama Sheria ya Madini na kanuni zake inavyofafanua.
Profesa Kikula aliongeza kuwa, wamiliki wa machimbo hayo wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na mpango wa huduma ya kwanza kwenye machimbo pamoja na kuhakikisha wachimbaji wanavaa vifaa vya kujikinga na madhara mbalimbali kwenye shughuli zao.
Wakati huohuo, Profesa Kikula alifanya ziara kwenye viwanda vidogo vya kufyatua matofali vya Vibrate Block na Nak Vibrate vilivyopo Wilayani Morogoro na kuwataka wamiliki wake kuhakikisha wananunua mchanga kwa wachimbaji wenye leseni za madini.
“Ikumbukwe tu kuwa ni kosa la kisheria kununua mchanga kwa mchimbaji asiye na leseni ya madini, adhabu yake ni faini pamoja na kutaifishwa kwa mchanga pamoja na vifaa,”alisisitiza Profesa Kikula.
Profesa Kikula alimwelekeza Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Morogoro (MOREMA), Dk. Omari Mzeru kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kutoa elimu kwa wachimbaji wa madini ya ujenzi kuhusu umuhimu wa kuendesha shughuli za madini kwa kuwa na leseni za madini, umuhimu wa kuwa na mpango wa utoaji wa huduma ya kwanza kwenye machimbo.
Wakizungumza katika nyakati tofauti wachimbaji wa madini ya ujenzi pamoja na wamiliki wa viwanda vidogo vya kufyatua tofali Wilayani Morogoro walimpongeza Profesa Kikula kwa kusikiliza na kutatua kero zao.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.