[Latest Updates]: Serikali Kutunga Kanuni Kuondoa Migongano ya Wenye Maduara na Wamiliki wa Leseni

Tarehe : June 23, 2024, 3 p.m.
left

-Eneo la Uwekezaji wa msaada wa kiufundi(Technical Support) kutengenezewa Kanuni

-Leseni za vikundi zilizotolewa na serikali kutouzwa bila ridhaa ya Tume ya Madini

-_Wachimbaji wapongeza hatua za Serikali za utatuzi wa kero

Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde amebainisha kwamba Serikali inajiandaa kutunga kanuni za kushughulikia migogoro kati ya wamiliki wa leseni na wenye maduara.

Waziri Mavunde Ameyasema hayo tarehe 22 Juni, 2024 Mkoani Shinyanga katika Kijiji cha Mandu, machimbo ya Ntambalale Wilayani Kahama alipotembelea kwa lengo la kutatua changamoto zinazowakabili wachimbaji wadogo.

"Mh.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuelekeza kuhakikisha tunatatua kero zote zinazowakabili wachimbaji wadogo ili wafanye shughuli zao bila migogoro yoyote. Na ndiyo maana, leo nimefika hapa kuja kuwasikiliza ndugu zangu ili kutatua changamoto zenu"

"Kufuatia migogoro ya kila wakati ya wenye Leseni kuanzia Julai 2024 tutaziangalia upya kanuni zetu. Tukikupa Leseni tunaamini wewe mmiliki wa leseni ndio mchimbaji. Iwapo mmiliki wa leseni yeyote ambaye atawakaribisha wachimbaji kwenye leseni yake, ahakikishe  anaingia mikataba itakayokuwa inatambua wenye maduara na uwekezaji waliouweka. Ikitokea mmiliki wa leseni anataka kuuza au kuingia ubia na mwekezaji, basi kila mmoja apate haki yake inavyostahili", alisisitiza Mhe. Mavunde.

Kuhusu msaada wa kiufundi (Technical Support) ambao uliwekwa kwa ajili ya kujenga uwezo kwa wachimbaji wadogo, Waziri Mavunde aliahidi kwamba Wizara inakwenda kuangalia vizuri Kanuni hizo ili ziweze kuendana na makusudio ya utungwaji wake.

Aidha, Mhe. Mavunde alibainisha kwamba msaada wa kiufundi ni lazima uendane na kuongeza matumizi ya teknolojia katika uchimbaji mdogo,  na si ilivyo sasa ambavyo inatafsiriwa kama ni kitendo cha kuuza leseni kwa wawekezaji na kuwaondoa wachimbaji wadogo huku matumizi ya teknolojia duni yakiendelea, hili haliwezekani na hatuwezi kulifumbia macho.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alionesha kutofurahishwa na jinsi leseni za vikundi zinavyouzwa pasipo idhini au makubaliano ya wanakikundi wote na kuahidi kwamba kuanzia Mwezi Julai, 2024 Leseni zote zitakazotolewa kwa vikundi kutoka Serikalini, hazitaruhusiwa kuingia mwekezaji pasipo kupata ridhaa kutoka kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, ili changamoto zisiendelee kujirudia.

Kuhusu suala la utoroshaji wa madini, Mhe. Mavunde aliahidi kuwa anakwenda kuongeza nguvu katika Mkoa wa Kimadini wa Kahama ili kuendelea kupambana na vitendo vya utoroshaji, kutokana na kwamba Kahama ni kama imekuwa kitovu cha vitendo vya utoroshaji wa madini.

Vilevile, Waziri Mavunde aliagiza kwamba Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi na Afisa Madini Mkazi wa Kahama wakae pamoja na kupitia tozo zote zilizoonekana kuwa kero ili kuondoa mzigo mkubwa kwa wachimbaji wadogo.

Mbunge wa Jimbo la Msalala Mh. Idd Kassim amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kusikiliza kero za wachimbaji na kuzipatia ufumbuzi na kutumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa jitihada zinazoendelea za kuboresha mifumo mbalimbali ya kuongeza ufanisi katika sekta ya Madini. 

Awali, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Mhandisi Joseph Kumburu akijibu baadhi ya hoja za wachimbaji aliahidi kwamba wataendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusiana na tozo na ushuru mbalimbali ambazo wanatozwa kwani zilizopo ni zile walizokubaliana kwa mujibu wa Sheria na si vinginevyo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mheshimiwa Anamringi Macha aliahidi kuendelea kusimamia maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali kwa lengo la kuimarisha utendaji wa sekta ya madini ambayo ni sehemu ya shughuli kuu za kiuchumi za Mkoa wa Shinyanga.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals