Tarehe : July 8, 2019, 5:49 a.m.
Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo leo tarehe 08 Julai, 2019 amefungua kongamano la madini linalowakutanisha wadau wa madini kwenye maonesho ya kimataifa ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kongamano hilo lilishirikisha Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Nchini (FEMATA), John Bina, Makamishna wa Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki na Haroun Kinega, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Michael Isamuhyo.
Wengine ni pamoja na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini, Dk. Venance Mwase, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Hamisi, wachimbaji na wafanyabiashara wa madini.
Lengo la kongamano hilo, lilikuwa ni kuwakutanisha wadau wa madini kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na kujadili chagamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya madini nchini na namna ya kuzitatua.
Naibu Waziri Nyongo alisema kupitia kongomano hilo, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Tume ya Madini pamoja na Taasisi nyingine zilizo chini yake, imejipanga kuhakikisha inapokea ushauri, maoni na mapendekezo yatakayowasilishwa ili kuboresha Sekta ya Madini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo alizitaka kampuni zinazojihusisha na uchimbaji wa madini kuwashirikisha wazawa kwenye utoaji wa huduma kwenye maeneo hayo kama mpango wa ushirikishwaji wa wazawa kwenye shughuli za madini (local content) unavyotaka.
“Kama Serikali ni lazima tujiridhishe kuwa watoa huduma wa ndani ya nchi wanatumiwa na kampuni za madini kabla ya kampuni kuanza kutumia watoa huduma wa nje ya nchi lengo ni kuhakikisha Sekta ya Madini inainua sekta nyingine muhimu,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Aidha, aliwataka watoa huduma wa ndani hususan kwenye mazao kuendelea kuboresha mazao yao ili kuhakikisha yanakidhi haja ya watumiaji katika Sekta ya Madini kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Nyongo alieleza kuwa, katika kuhakikisha sekta ya madini inakua kwa kasi na kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, mnamo Januari 22, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli alifanya mkutano na wadau wa madini nchini jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kusikiliza na kutatua kero za wadau wa madini.
Alieleza kuwa, miongoni mwa kero zilizopatiwa ufumbuzi kutokana na mkutano huo ni pamoja na kuondolewa kwa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya asilimia 18 na kodi ya zuio ya asilimia tano na uanzishwaji wa masoko ya madini.
Aliongeza kuwa, katika kuhakikisha rasilimali za madini zinakuwa na manufaa kwa wananchi hasa wa kipato cha chini pamoja na kuondoa kero ya kukosekana kwa masoko ya madini na kuondoa changamoto ya utoroshwaji wa madini nchini, Wizara kwa kushirikiana na Tume ya Madini imerahisisha biashara ya madini kwa kuratibu uanzishwaji wa masoko ya madini 29 ambayo yanafanya vizuri.
Wakati huohuo, Nyongo alitoa wito kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kutumia masoko yaliyoanzishwa na wale wasio waaminifu kuacha kutorosha madini kwani kwa kufanya hivyo watapata hasara ya kupigwa faini na madini hayo kutaifishwa.
Aliitaka TANTRADE kuendelea kuwakutanisha wadau wa madini wa ndani ya nchi na wa nje ya nchi lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na teknolojia kwenye shughuli za madini.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Nchini (FEMATA), John Bina akizungumza katika kongamano hilo, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Madini kwa kuendelea kutatua changamoto zao zilizoainishwa na wadau wa madini kwenye mkutano wao na Rais John Magufuli tarehe 22 Januari, 2019 jijini Dar es Salaam
Bina aliiomba TANTRADE kuwafikia wachimbaji wote kwenye maeneo yao na kuwaunganisha na wachimbaji wa nje ya nchi lengo likiwa ni kukuza masoko na teknolojia.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo alisema kuwa shirika hilo lipo tayari kushirikiana na TANTRADE katika kuwasaidia wachimbaji wadogo.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.