[Latest Updates]: Mavunde Abainisha Dira Sekta ya Madini Kuelekea 2030

Tarehe : Sept. 11, 2023, 11:29 a.m.
left


#Aanisha Mikakati  katika Sekta ya Madini

#Asisitiza kuijengea uwezo GST kufanya Utafiti wa kina

#Aeleza Madini Mkakati kulibeba Taifa

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde ameainisha vipaumbele vyake katika Sekta ya Madini ili kuhakikisha taifa linanufaika na uwepo wa Madini yanayopatikana hapa nchini.

Ameainisha hayo  septemba 11 , 2023 wakati akizungumza katika Mkutano  wa  Wachimbaji Wadogo wa Madini kutoka   Shirikisho la  Wachimbaji wadogo wa  Madini Tanzania (FEMATA) uliofanyika jijini Dodoma. 

Akizungumzia juu ya kuongeza taarifa za utafiti wa  jiolojia Mhe.Mavunde amesema  kuwa moja ya vipaumbele vyake katika sekta ya madini ni kuijengea uwezo Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ili iweze kufanya utafiti wa kina kwa ndege yaani (Air Born Geophysical Survey) utakaotoa taarifa zitaonesha utajiri wa madini yaliyopo nchini kwa kiwango kikubwa tofauti na sasa ambapo ni  asilimia 16 tu ya eneo lote nchi nzima limefanyiwa utafiti wa kina.

Waziri Mavunde ameongeza kuwa GST inapaswa kufanana na taasisi nyingine za Utafiti wa Madini duniani ikiwa na  maabara ya kisasa itakayotumiwa na wachimbaji wote nchini.

“Ndugu zangu tukipiga picha ya miamba yote nchi nzima, tutapata taarifa sahihi ya kijiolojia ili wachimbaji wasifanye kazi zao kwa kubahatisha , uchimbaji ni Sayansi sio bahati wala uchawi, mchimbaji mwenye taarifa  ya utafiiti wa kijiolojia atafanikiwa zaidi kupitia Sekta hii ya Madini” amesema Mavunde. 

Akielezea faida za utafiti huo Mhe. Mavunde amesema taarifa wa kina wa  jiolojia utaleta tija na mapinduzi makubwa katika sekta  nyingine akitolea mfano sekta ya kilimo hasa katika utafiti wa udongo,mbolea na sekta ya  maji katika uchimbaji visima.

Aidha, ametaja mpango mwingine kuwa Wizara itaenda kuwa na makumbusho ya madini  ili wananchi wapate kuona na kufahamu madini yanayopatikana  nchini kuliko kuyasikia tu.

Akizungumzia kuhusu utoroshaji wa madini Mhe. Mavunde amesema serikali ipo macho muda na mpango mkubwa ni kutokomeza utoroshaji wa madini nchini ili madini yote yaliyopo kwenye mnyororo wa biashara ya madini yaonekane na yalete faida kwa taifa.

Amesema kuwa mtihani wake wa kwanza kama Waziri wa Madini ni kuhakikisha Wizara inakusanya shilingi trilioni 1 kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 hivyo suala la utoroshaji madini halina nafasi. 

“Kuhusu utoroshaji naomba tushirikiane ntasimamia sheria,  sitasita kuwachukulia hatua wale wote wanatorosha madini, sitaangalia sura ya mtu, nitahakikisha nasimamia kwa dhati na naamini kwa kushirikiana tutafanikisha kumaliza kabisa hilo tatizo, mimi na wenzangu tutakuwa wakali sana katika hili, milango yangu itakuwa wazi tushirikiane,” amesema Mavunde. 

Akielezea kuhusu migogoro  Mhe .Mavunde ameongeza kuwa hatasikiliza mgogoro wowote wa maeneo ya madini ambao haujapitia ngazi ya mikoa husika, na kwamba migogoro hiyo isikilizwe katika maeneo na pale inaposhindikana itapewa rufaa na  kusikilizwa hatua inayofuata.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde ameeleza kuwa ipo changamoto ya Wachimbaji wa Madini ya Dhahabu wengi wao kutopeleka dhahabu kwenye viwanda vya kusafishia dhahabu hivyo katika kutatua hilo, Serikali itatoa mikopo kupitia wamiliki wa viwanda hivyo ili wachimbaji wanapokuwa na dhahabu zao wapeleke kusafisha kwenye viwanda hivyo ili kuongeza mzunguko wa fedha.

Amesema kuwa katika kutatua shida ya mitaji tayari Wizara imeongea na Shirikisho la Mabenki Tanzania  (TBA) na wametoa ahadi kwamba watakaa kikao na Wachimbaji wa Madini ili kujua mnyororo mzima wa biashara hiyo na hatimaye watoe mikopo kwa ajili ya kuwapa mitaji Wachimbaji wa Madini.

Pia, Waziri Mavunde amesema kuwa Serikali kupitia Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) imeleta mashine 5 za uchorongaji na lengo ni kuwa na mashine 15 za uchorongaji kufikia mwezi Juni 2024, kwa ajili  kuwasaidia Wachimbaji Wadogo. 

Akizungumzia  Madini ya Kimkakati Mhe. Mavunde amesema kuwa kwa mwelekeo wa dunia ya sasa madini hayo yanakwenda kuwa na soko kubwa na kwamba Tanzania haitajiweka kando, kwa kuwa mtizamo wa dunia ni kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kutumia nishati safi.

“Madini ya Kimkakati, mahitaji ya dunia leo ni tani milioni 10, kufikia mwaka 2050 mahitaji yatakuwa tani tani laki 1 na nusu, sisi Tanzania tunabahati na kuwa nayo, tunaenda kuyapa kipaumbele ili utajiri huu tunufaike nao" amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini,  Dkt. Steven Kiruswa amewasihi Wachimbaji, Wafanyabiashara na watu wote wanaojihusisha na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini kufuata utaratibu kwa kulipa kodi sambamba na kuepuka utoroshaji Madini ili Sekta ilifikie lengo lake kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa. 

Awali, akizungumza katika kikao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,  Kheri Mahimbali alieeleza kuwa  Kwa mujibu wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 Sekta ya Madini inatarajia kuchangia asilimia 10 kwenye Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 ambapo Mpaka kufikia mwaka 2022 Sekta ya Madini imechangia asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa.

Naye, Rais FEMATA John Bina, amesema kuwa Mchango wa Wachimbaji Wadogo umefikia asilimia 40 katika Sekta ya Madini kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Madini kwa mwaka wa 2022/2023 ilinganishwa na mchango wa asilimia 8 tu ya mwaka 2016/2017.

Ameiomba serikali kupunguza kodi  katika mitambo inayoingizwa hapa nchini kwa ajili ya kurahisisha uchimbaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa zaidi. 

Aidha, Bina ameongeza kuwa FEMATA kwa kushirikiana na STAMICO wako kwenye hatua za mwisho za mchakato wa kuanzisha benki kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo nchini.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals