[Latest Updates]: Mwenyekiti Tume ya Madini, atatua mgogoro sugu wa madini, Nzega

Tarehe : Nov. 29, 2018, 9:21 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Nzega

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula leo tarehe 06 Desemba 2018 ametatua mgogoro uliodumu kwa muda mrefu kati ya vikundi viwili vilivyokuwa vinajishughulisha na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu katika eneo la Mwamikola lililopo Wilayani Nzega mkoani Tabora.

Mmiliki wa eneo lililopo katika kijiji cha Mwamikola kilichopo katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, Rashid Kavula ( kushoto) pamoja na Katibu wa Kikundi cha wachimbaji wa madini ya dhahabu kilichokuwa kinaendesha shughuli zake za madini katika eneo hilo cha Mwaguguli Mining Society, Nyansaho Sumar (kulia) wakishikana mikono kama ishara ya kumaliza mgogoro baina yao kwenye mkutano wa wachimbaji wadogo wa madini uliofanyika katika kijiji hicho.[/caption]

Vikundi hivyo ni pamoja na kikundi cha Mwaguguli Mining Society na kikundi cha Mwamikola Gold Mining Society ambapo mgogoro wao ulitokana na mwingiliano wa maombi ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini.

Profesa Kikula aliyekuwa Wilayani Nzega kwa ajili ya kutatua mgogoro huo aliambatana na watendaji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kamishna kutoka Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki, Meneja wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Zephania Maduhu na Mwanasheria kutoka Tume ya Madini, Hadija Ramadhani.

Wengine waliokuwepo katika ziara hiyo ni pamoja na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Mayigi Makolobela, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega, Onesmo Kisoka, Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya pamoja na waandishi wa habari.

Mara baada ya kufanya mazungumzo na pande zote mbili kwa pamoja, Profesa Kikula alitoa maelekezo kulingana na sheria ya madini  kwa kusema kuwa maombi ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society hayakustahili kupewa leseni  kwa kuwa yameombwa  kabla ya leseni iliyokuwepo kumaliza muda wake kinyume na Kifungu cha 15(2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake ya Mwaka 2017.

Profesa Kikula aliongeza kuwa ombi la kikundi cha Mwamikola Gold Mining Society linastahili kupewa leseni kwa vile liliombwa baada ya leseni ya awali  kumaliza muda wake na kuongeza kuwa, baada ya maombi ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society kukataliwa kupewa leseni, kulingana na Sheria ya Madini kikundi husika kinaweza kuomba tena eneo  ambalo haliingiliani na eneo la ombi la Mwamikola Gold Mining Society.

Awali akielezea historia ya mgogoro huo, Profesa Kikula alisema kuwa mgogoro huo uliopo katika kijiji cha Mwamikola, Kata ya Mwangoye Wilayani Nzega mkoani Tabora ulitokana na mwingiliano wa maombi ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini.

Alisema maombi ya vikundi hivyo kwa ajili ya uchimbaji wa madini yaliombwa katika eneo la leseni  ya utafutaji wa madini ya kampuni ya Resolute Tanzania Limited iliyotolewa Machi 14, 2014 na kumaliza muda wake Julai 13, 2018.

Kamishna kutoka Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki (kulia) akifafanua jambo kwa wachimbaji wa madini katika machimbo ya dhahabu yaliyopo katika kijiji cha Mwamikola kilichopo Wilayani Nzega mkoani Tabora. Katikati ni Meneja wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Zephania Maduhu[/caption]

Aliendelea kusema kuwa eneo linaloombewa leseni lilivamiwa na wachimbaji wadogo  mwezi Januari, 2017 na kuongeza kuwa Tume ya Madini ilisimamisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo mapema Agosti mwaka huu kufuatia kuibuka kwa mgogoro  baada ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao.

Aliendelea kueleza kuwa Septemba 13 mwaka huu, Tume ya Madini ilituma wataalam wake kufanya ukaguzi katika eneo la mgogoro na kuonekana kuwa mgogoro husika ulitokana na wachimbaji waliovamia eneo hilo kugawanyika na kuunda vikundi viwili ambavyo vimeomba leseni ndogo ya uchimbaji wa madini.

Profesa Kikula aliendelea kufafanua kuwa, kikundi cha Mwaguguli Mining Society kiliwasilisha maombi yake ya leseni  tatu za  uchimbaji mdogo wa madini  Julai 13, 2018 huku kikundi cha Mwamikola Gold Mining Society kikiwasilisha maombi ya leseni ya uchimbaji mdogo wa madini katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora katika eneo lililokuwa linachimbwa wakati wa uvamizi Agosti 06, 2018.

Alisisitiza kuwa ilionekana sehemu ya eneo la maombi ya kikundi cha Mwaguguli Mining Society inaingiliana na eneo la ombi la kikundi cha Mwamikola Gold Mining.

Katika hatua nyingine, Profesa Kikula alisema Serikali kupitia Tume ya Madini ipo tayari kusaidia vikundi vyote katika maombi mapya ya leseni za uchimbaji mdogo wa madini kwa haraka ili waweze kuendelea na shughuli za uchimbaji wa madini na kujipatia kipato huku Serikali ikipata mapato yake stahiki.

Alimwagiza Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Mayigi Makolobela kuhakikisha anasaidia kwa haraka vikundi husika katika upatikanaji wa leseni mpya za uchimbaji mdogo wa madini ili waendelee na shughuli za uchimbaji wa madini na kukuza uchumi wao uliokuwa umesimama kutokana na usitishwaji wa shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo husika kutokana na mgogoro.

Meneja wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Zephania Maduhu (kulia) na Mwanasheria wa Tume hiyo, Hadija Ramadhan (kushoto) wakibadilishana mawazo kabla ya kuanza kwa ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.[/caption]

Wakizungumza katika nyakati tofauti mara baada ya maamuzi kutolewa na Serikali kupitia Tume ya Madini, viongozi wa vikundi husika waliipongeza Tume ya Madini kwa utatuzi wa mgogoro kwa kuwa walikuwa wameathirika kiuchumi mara baada ya shughuli za uchimbaji wa madini kusimamishwa kutokana na mgogoro husika.

Naye Mfadhili wa kikundi cha Mwaguguli Mining Society, Shukrani Chacha mbali na kuridhika na kupongeza uamuzi uliotolewa na Tume ya Madini aliomba wachimbaji kutoka katika kikundi cha Mwamikola Mining Society kuzika tofauti zao na kuanza upya ushirikiano ili kila kikundi kinufaike na rasilimali za madini.

Aliongeza kuwa mgogoro uliodumu kwa kipindi kirefu haukuwa na tija kwenye uzalishaji badala yake ulipelekea uchumi katika kijiji cha Mwamikola kudorora na kusisitiza kuwa anaamini mara baada ya kuanza upya kwa shughuli za uchimbaji wa madini uchumi utakua kwa kasi.

Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Mwamikola Gold Mining Society, Princh Kissoro aliongeza kuwa utatuzi wa mgogoro umewapa ari mpya ya kufanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo husika mara baada ya kupata leseni mpya za uchimbaji mdogo wa madini.

Wakati huo huo Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Mayigi Makolobela alisema kuwa atahakikisha vikundi husika vinawasilisha maombi yao upya na kupatiwa leseni ndani ya muda mfupi ili waendelee na uchimbaji wa madini.

Makolobela aliwataka wachimbaji wadogo katika mkoa wa Tabora kuomba leseni kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano muda wowote kwa wachimbaji wadogo wa madini.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals