[Latest Updates]: Mgodi wa Kiwira waanza kuchenjua makaa ya mawe

Tarehe : Nov. 29, 2018, 9:16 a.m.
left

Na Asteria Muhozya, Kiwira

Waziri wa Madini Angellah Kairuki amesema ipo fursa kubwa katika Migodi ya Kiwira na Kabulo inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na tayari Serikali kupitia shirika hilo, imeanza kufufua baadhi ya mitambo  mgodini hapo ikiwemo ya kuchakata madini hayo.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia vumbi linalotokana na shughuli za uchimbaji wa makaa katika eneo la Kabulo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli a uchimbaji makaa ya mawe na Shirika la Madini la Taifa, (STAMICO)[/caption]

Waziri Kairuki aliyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea katika migodi hiyo mwishoni mwa wiki na kuchukua fursa hiyo kuwapongeza watumishi wa Kiwira kutokana na  uzalendo waliouonesha kuhakikisha kwamba mgodi huo unafanya kazi tena.

Aliongeza kwamba, migodi ya Kiwira na Kabulo ni migodi inayotegemeana   hivyo serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba machimbo ya chini katika mgodi  wa Kiwira yananza uzalishaji na ikiwezekana kufikia mwakani uzalishaji kupitia machimbo hayo ufanyike kwa asilimia 100.

Akizungumzia madai ya wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira, alisema tayari madeni hayo yamekwishaanza kulipwa kila uzalishaji unapofanyika na kuongeza, “ madeni ya watumishi yataendelea kulipwa kila wakati uzalishaji unapofanyika hivi ndivyo tulivyokubaliana’’.

Aidha, Waziri Kairuki alimtaka  Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, kuona namna ya kutoa motisha kwa wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira hususan wale wanaokaribia kustaafu ikiwa ni ishara ya kuthamini michango yao kwa kutumikia mgodi huo kwa uzalendo na moyo wa kujitolea.

Wakati huohuo, akizungumza katika eneo la machimbo ya Kabulo, alisema kuwa, mgodi huo ulisimama kwa kipindi kirefu hivyo jitihada za serikali ni kuhakikisha kwamba unaanza tena kufanya kazi ili kuleta tija kwa taifa ikiwemo serikali kupata mapato.

Aliongeza kuwa,  wizara  inafanya mashauriano na Wizara ya Nishati ili kuna namna ambavyo makaa ya mawe katika machimbo ya Kiwira na Kabulo yanaweza kutumika kuzalisha umeme  utakaoingizwa  katika gridi ya taifa  na kueleza, “tutakapokuwa tayari tutaanza kuzalisha megawati 200,”.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira[/caption]

Akizungumzia hali ya uzalishaji  alisema kwamba,  katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba,2018, mgodi wa Kabulo umezalisha tani  Laki Mbili na mbili elfu  ambazo ni mara mbili ya kile kilichozalishwa mwaka jana na kuongeza kwamba,  tayari tani elfu 37 zimesafirishwa nje ya nchi.

Aidha, alisema mkakati  wa wizara ni kuongeza matumizi ya makaa ya mawe  na kuutaja mkakati wa kutumia makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani ili kuwezesha matumizi ya makaa ya mawe kutumika majumbani badala ya mkaa ambao unaharibu misitu.

“Tunaishukuru kampuni ya SMG kuingia kandarasi na STAMICO katika kuchimba madini haya Kabulo,” alisema Kairuki.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Madini la Taifa ((STAMICO), Kanali Mhandisi Syvester Ghuliku, alisema kuwa shirika hilo limefanya ukarabati wa mtambo wa kuchenjua makaa ya mawe katika mgodi wa Kiwira ambao umegharimu shilingi milioni 30 pamoja na kufanya ukarabati wa maabara na kununua vifaa ambavyo vimegharimu shilingi milioni 12 na kuongeza kuwa, hayo yote yamefanyika ili  kuweka thamani ya madini hayo.

Akizungumzia mipango ya shirika alileza kwamba ni kuendelea kuboresha miundombinu ya mgodi huo kadri uzalishaji unapofanyika likilenga kuhakikisha kwamba mgodi huo unarejesha uzalishaji wake kama ilivyokuwa awali.

Akizungumzia  hali ya uzalishaji katika machimbo ya  Kabulo alisema wateja wa makaa hayo wamekuwa ni viwanda vya saruji , viwanda  vya uzalishaji , nchi za  Kenya na Rwanda na kuongeza kuwa, wateja zaidi wanatarajia kuongezeka kadri uzalishaji unavyoendelea na kuongeza.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akipata ufafanuzi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa ( STAMICO), Kanali Mhandisi Syvester Ghuliku wakati wa wa ziara yake alipotembelea mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira.[/caption]

Akizungumzia manufaa kwa wananchi wa Kabulo alisema wananchi wanaozunguka migodi hiyo wamenufaika kwa kupata ajira ndogo ndogo na pia wanatarajia kunufaika pale mradi wa makaa ya mawe kwa ajili ya matumizi ya majumbani utakapoanza.

Aidha, alisema kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Ileje inanufaika kutokana na kuwepo kwa mgodi wa Kabulo kutokana na tozo zinazolipwa.

Naye, Meneja uzalishaji  na Msimamizi wa Migodi ya Kiwira na Kabulo  Peter Maha, alieleza kuwa, mgodi huo unatarajia kuongeza   uzalishaji  wa makaa ya mawe  ikiwemo kuongezeka kwa  idadi ya wateja  wakiwemo wateja wa zamani ambao walikuwa wakipata makaa hayo kutoka mgodi huo na  kuongeza “ Hata  viwanda vipya sasa vitakuwa na uhakika wa nishati kutokana na makaa tunayoyazalisha hapa,”

Nao, wafanyakazi wa mgodi wa Kiwira wakizungumza katika kikao baina yao na Waziri Kairuki, waliitaka serikali kuhakikisha inaufufua mgodi huo kutokana na  manufaa yake kwa taifa na hususan katika kipindi hiki ambacho kipaumbele cha serikali ni kuwa na Tanzania ya Viwanda na kuongeza, yapo manufaa makubwa kwa taifa kupitia madini ya makaa ya mawe ikiwa mgodi huo utarejesha shughuli zake za uzalishaji kama ilivyokuwa hapo awali.

Pia, waliitaka wizara isaidie kuhakikisha kwamba inakifufua kituo za zamani   cha kuzalisha  umeme mgodini hapo  wakati ikijipanga kujenga kituo kipya kutokana na kwamba, endapo nishati hiyo itazalishwa moja kwa moja mgodini hapo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals