[Latest Updates]: Tanzania Yapata Nafasi Muhimu Kongamano la Lithium Ujerumani

Tarehe : Dec. 6, 2023, 7:03 p.m.
left

Yatajwa kama Mdau Muhimu kuzalisha Madini ya Nishati Safi

Dodoma na Halle- Ujerumani

Wizara ya Madini imepata fursa muhimu ya kutangaza Madini ya Lithium na Madini mengine Mkakati ambayo nchi imebarikiwa kuwa nayo katika Kongamano la LithiumDays23 linalofanyika kila mwaka mjini Halle nchini Ujerumani.

Katika kongamano hilo, Tanzania imepewa heshima ya kushiriki kwa njia ya mtandao na ana kwa ana ambapo Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini  Augustine Olal  kwa niaba ya Katibu Mkuu amewaongoza  Wataalamu wa Wizara kushiriki kwa njia ya mtandao kutoka  Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.

 Aidha, katika kongamano hilo, Tanzania imepata nafasi  muhimu ya kujitangaza kama nchi ijayo mshirika wa LithiumDays24 na mwandaaji mwenza wa kongamano hilo.

Akitoa wasilisho katika kongamano hilo, Olal  amesema nchi ya Tanzania inao utajiri wa urithi wa kijiolojia unaofanana na nchi ya Congo DRC ambayo ni mzalishaji mkubwa wa madini muhimu na mkakati na kueleza kwamba, hiyo ni kiashiria tosha kuwa Tanzania inaweza kuwa  mzalishaji mkubwa wa madini hayo ambayo kwa kiasi kikubwa bado hayajaguswa. Hivyo, uwekezaji unahitajika katika kutafiti na kuchimba madini hayo.

‘’Amana kubwa za madini ya lithium nchini Tanzania pamoja na akiba kubwa ya madini ya kobati na nikeli zinaiweka Tanzania kama mdau wa kimkakati katika mnyororo wa kimataifa wa mzalishaji wa madini kwa ajili ya magari ya kutumia umeme na suluhu ya nishati safi,’’ amesisitiza Olal.

Amewahakikishia kuwa, Serikali inayo dhamira ya dhati katika kukuza mazingira rafiki ya  uwekezaji na inashiriki kikamilifu katika mageuzi ya Sera na maendeleo ya miundombinu ili kuwezesha uchimbaji wa madini hayo muhimu.

Pia, Olal ameongeza kuwa,  kutokana na  amani iliyopo nchini na usalama ni hakikisho tosha kwamba Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza katika Ukanda wa Afrika Mashariki  na kusema inayo heshima kubwa kuwa sehemu ya kongamano hilo na inatazamia kuwa mshirika muhimu katika uendelezaji wa madini hayo.

 Awali, akimkaribisha  Kaimu Katibu Mkuu kutoa wasilisho katika kongamano hilo, mwandaaji mwenza wa kongamano hilo kutoka Taasisi ya Teknolojia na Uchumi wa Lithium, Halle nchini Ujerumani Prof. Dr. Gregor Borg ameielezea Tanzania kama mdau muhimu katika uzalishaji wa madini ya nishati safi na nchi iliyobarikiwa kwa utajiri wa madini mbalimbali. 

Profesa Borg pia amewahi  kushiriki katika shughuli nyingi za utafiti wa madini nchini Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

Kongamano la Lithium Days ni jukwaa linalotumika kubadilishana mawazo na maendeleo ya utafiti yanayohusu teknolojia ya lithium na madini mengine mkakati na matumizi yake.

 Aidha, kongamano hilo huwaleta pamoja wataalam wa utafiti wa sekta ambao wanalenga kutafiti na kufanya ufumbuzi endelevu na ubunifu  kuhusiana na hifadhi ya nishati ya umeme.

Vilevile, LithiumDays hutumika kama kitovu muhimu cha kuendeleza utafiti unaohusiana na litihium hatimaye kuchangia katika maendeleo ya vyanzo vya nishati safi na kusaidia juhudi za kimataifa na mabadiliko ya tabia nchi.

 Tanzania inajiandaa kikamilifu kuhakikisha inakuwa miongoni mwa nchi wazalishaji wa madini ya lithium na mengine ya kimkakati kutokana na mahitaji makubwa ya madini hayo duniani katika siku za usoni .
 Kwa upande wa Tanzania, kutokana na tafiti za awali zinaonesha uwepo wa  madini ya Lithium kwa kiasi kikubwa katika Mkoa wa  Dodoma.

Kampuni kadhaa ambazo zimeorodheshwa katika Soko la Hisa la nchini Australia zijulikanazo kama Liontonwn Resources  Ltd (ASX: LTR) Cassius Mining Limited (ASX: CMD) Intra Energy Corporation Limited (ASX:IEC) na Auroch Minerals (ASX: AOU) zilizoonesha nia  kutafiti madini ya lithium mkoani Dodoma, matokeo ya utafiti wake  wa awali yalionesha matokeo chanya.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals