[Latest Updates]: Leseni za madini kuanza kutolewa muda wowote

Tarehe : May 8, 2018, 10:13 a.m.
left

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa zoezi la utoaji wa leseni kwa ajili ya utafiti, uchimbaji na biashara ya madini linatarajiwa kuanza muda wowote kuanzia sasa mara baada ya uanzishwaji wa Tume ya Madini.

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (katikati waliokaa mbele), Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ( wa nne kutoka kulia waliokaa mbele), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini ( wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wote mara baada ya uzinduzi wa mkutano huo.

Profesa Msanjila ameyasema hayo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari  kwenye mkutano wa baraza la kwanza la  wafanyakazi wa Wizara ya Madini mjini Morogoro  tarehe 07 Mei, 2018 wenye lengo la kujadili utendaji kazi na namna ya kukabiliana na changamoto katika sekta ya madini.

Akielezea hatua iliyofikiwa ya zoezi hilo, Profesa Msanjila amesema kinachofanyika kwa sasa ni uchambuzi wa maombi ya leseni zote zilizokwishawasilishwa na kampuni mbalimbali zenye lengo la kujihusisha na shughuli za madini nchini.

Katika  hatua nyingine, akielezea mkutano huo, Profesa Msanjila amesema mkutano huo wa kwanza unaambatana na uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi ambalo lipo kisheria.

Ameendelea kueleza kuwa masuala yatakayojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na umuhimu wa baraza la wafanyakazi, muundo wa Wizara ya Madini na maadili katika utumishi wa umma.

Ametaja masuala mengine kuwa ni pamoja na mapitio na utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018, mpango wa bajeti wa mwaka 2018/2019 na marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula amesema kuwa tayari tume imekaa na kuweka mkakati  kuhusu masuala ya leseni ili kuhakikisha kuwa leseni zinatolewa kwa wakati baada ya  zoezi la utoaji wa leseni kusitishwa tangu Julai mwaka 2017.

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula akitoa ufafanuzi katika mkutano huo

Akielezea hatua iliyofikiwa ya zoezi la uchambuzi wa leseni, Profesa Kikula amesema zaidi ya leseni 8,000 zimeshachambuliwa na kusisitiza kuwa zoezi litakapokamilika  waombaji waliokidhi vigezo watataarifiwa ili  kuanza kufanya taratibu za malipo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Agathon William amesema kuwa baraza la wafanyakazi ni chombo  muhimu kinachowaunganisha wafanyakazi wa Wizara katika uongozi kwa pamoja mahali pa kazi ili kuleta tija katika utekelezaji wa shughuli za Wizara.

Amesema baraza huishauri Wizara juu ya kuongeza ufanisi wa kazi na hatua zinazofaa kuchukuliwa kuhakikisha kuwa huduma zitolewazo na Wizara ni za kuridhisha kulingana na malengo ya Taifa ya kuleta maendeleo na kupunguza umaskini kwa kuanzisha viwanda vingi vitakavyoongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi wa Taifa.

Ameendelea kusema kuwa baraza hilo hujadili na kushauri mipango na bajeti ya wizara na kupima mafanikio na kuridhia utekelezaji wake pamoja na upandishwaji wa vyeo wafanyakazi kutokana na miundo ya utumishi.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase na Asteria Muhozya, Morogoro

Maafisa Habari,

Wizara ya Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@madini.go.tz,                                                                               

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals