[Latest Updates]: Naibu Waziri Biteko atatua mgogoro machimbo ya madini Bunda

Tarehe : Oct. 1, 2018, 7:47 a.m.
left

  • Atoa miezi miwili kwa mwekezaji kulipa fidia wananchi

Na Greyson Mwase, Bunda

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ametatua mgogoro mkubwa wa siku nyingi uliokuwepo kati ya wananchi wa kijiji cha Kunanga kilichopo ndani ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara na kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Lake Victoria kwa kuitaka kampuni  kuhakikisha imelipa fidia kwa wananchi wote ndani ya  kipindi cha miezi miwili.

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kunanga kilichopo katika wilaya ya Bunda mkoani Mara. (hawapo pichani)[/caption]

Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo leo tarehe 21 Septemba, 2018 mara baada ya kufanya ziara kwenye machimbo na kusikiliza kero za wachimbaji wadogo kupitia mkutano wa hadhara ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Mara na Geita yenye lengo  la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja kusikiliza na kutatua kero mbalimbali.

Ziara hiyo katika machimbo hayo inatokana na maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliyoyatoa katika mkoa wa Mara kwenye ziara yake  aliyoifanya kuanzia tarehe 05 hadi 07 Septemba  mwaka huu ya kumtaka Naibu Waziri wa Madini kuhakikisha ametatua mgogoro husika.

Katika ziara hiyo, Biteko aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili, Rais wa Chama cha Wachimbaji Madini Nchini, John Bina, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mara, Stephan Msseti, Mbunge wa Bunda Vijijini, Boniphace Getere, Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya, Watendaji kutoka Wizara ya Madini pamoja na waandishi wa habari.

Alisema kuwa, baada ya kusikiliza maelezo kutoka pande zote mbili alibaini kuwa wanachi walikuwa na haki ya kulipwa fidia na kumtaka mwekezaji kuhakikisha kuwa anafuata sheria na kanuni za madini kwa kuhakikisha amefanya tathmini na kuwalipa fidia ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Aliendelea kufafanua kuwa, zipo taratibu zinazotakiwa kufuatwa na wawekezaji wote kwenye madini ikiwa ni pamoja na kujitambulisha kwa Wakuu wa Wilaya, Vijiji na wananchi na kufanya mazungumzo na kuweka makubaliano ya fidia pamoja na kulipa kabla ya kuanza rasmi shughuli za uchimbaji madini.

“Haiwezekani kamwe mwekezaji anapewa leseni na Ofisi ya Madini anakwenda moja kwa moja kwa wananchi tena akiwa na walinzi na kuanza kuwafukuza bila hata kujitambulisha na kufanya mazungumzo, hii inahatarisha usalama na uhusiano kati ya mwekezaji na wananchi wa sehemu husika,” alisema Naibu Waziri Biteko.

Mkuu Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili akifafanua jambo kwenye mkutano wa hadhara[/caption]

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Mkurugenzi wa kampuni ya uchimbaji wa dhahabu ya Lake Victoria, Ahmed Magoma na Mkuu wa  Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili kufanya mkutano na wananchi ili kutafuta mustakabali wa fidia na kumpatia taarifa.

Aidha, alimtaka  mwekezaji kuomba kikao na Serikali ya Kijiji kabla ya siku ya Jumatano ya wiki ijayo ya tarehe 26 Septemba mwaka huu na kuendelea kumtaka kuhakikisha anashirikiana na wananchi kwa karibu zaidi na kudumisha mahusiano.

Pia Waziri Biteko alimtaka mwekezaji kuhakikisha analipa deni la Dola za Kimarekani 46,080  Serikalini ndani ya kipindi cha siku 45 tangu alipoandikiwa hati ya makosa kama mojawapo ya uvunjifu wa sheria ya madini pamoja na kanuni zake.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Biteko alimtaka Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya kuhakikisha eneo lililobaki lenye ukubwa wa kilomita za mraba 5.12 lililotolewa na mwekezaji linagawanywa na kupewa kwa wachimbaji wadogo wa madini.

Katika hatua nyingine, akiwa katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko alisikitishwa na kitendo cha wachimbaji wadogo wa madini kutokulipa mrabaha serikalini hali inayoikosesha Serikali mapato yake stahiki.

Alielekeza Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili na Mwenyekiti wa kijiji cha Kunanga, Kisire Marwa kukaa kwa pamoja na kuchunguza kiasi cha fedha zinazodaiwa kulipwa na wachimbaji wadogo wa madini katika serikali ya kijiji na matumizi yake na kisha kutoa taarifa kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Lake Victoria, Ahmed Magoma akielezea historia ya mgogoro kati ya kampuni yake na wananchi wa kijiji cha Kunanga kilichopo katika wilaya ya Bunda mkoani Mara kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko. (hayupo pichani)[/caption]

“Wachimbaji hawa wanadai kuwa  wanalipa fedha katika serikali ya kijiji, kiasi halisi hakijulikani wala matumizi yake, fedha hizi zinatakiwa ziwanufaishe kupitia uboreshaji wa huduma za jamii,” alisema Biteko.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haipo tayari kuona mwekezaji au mchimbaji yeyote ananyanyasika na kufafanua kuwa kila mwananchi ni sehemu ya rasilimali za madini.

Pia, aliwataka wananchi kutii sheria ya madini pamoja na kanuni zake na kuongeza kuwa wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye shughuli za utafutaji na uchimbaji madini.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Lake Victoria, Ahmed Magoma akizungumza mara baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri Biteko, aliomba msamaha kwa wananchi wa kijiji cha Kunanga na kueleza kuwa atatekeleza maelekezo yote ikiwa ni pamoja na kuimarisha mahusiano kati yake na wananchi husika ili uchimbaji wa madini ufanyike kwa amani na kila upande uweze kufaidika

Naye Mkuu wa  Wilaya ya Bunda, Mwl. Lidia Bupilipili pamoja na pongezi kwa Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema kama serikali watafuatilia kwa karibu mapato na matumizi  ya fedha zinazodaiwa kulipwa katika serikali ya kijiji cha Kunanga na kuchukua hatua kwa waliohusika na ufujaji wa fedha hizo.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals