[Latest Updates]: Waziri Biteko azitaka kampuni za madini kuwasilisha mipango ya ufungaji wa migodi

Tarehe : Dec. 16, 2019, 8:39 a.m.
left

Na Greyson Mwase, Dodoma

Waziri wa  Madini, Doto Biteko ameziagiza kampuni za madini nchini  zinazojihusisha na uchimbaji wa kati na mkubwa kuwasilisha mipango ya ufungaji wa migodi kama  Sheria ya Madini na kanuni zake inavyoelekeza.

Waziri Biteko aliyasema hayo leo tarehe 16 Desemba, 2019 kwenye kongamano la kwanza la usimamizi na utunzaji endelevu  wa mazingira katika Sekta ya Madini jijini Dodoma linalokutanisha kampuni za madini,  taasisi za serikali na wataalam wa mazingira kutoka taasisi mbalimbali lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu kwenye usimamizi wa mazingira.

Viongozi wengine walioshiriki katika kongamano hilo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,  Profesa Simon Msanjila, Kamishna wa Madini Nchini, Mhandisi David Mlabwa, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya, Kamishna kutoka Tume ya Madini ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Nchini (FEMATA), Haroun Kinega na Watendaji kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.

Alisema kuwa, kwa hapa nchini kuna wamiliki wa migodi mikubwa  na ya kati takribani 200 ambao wanastahili kuwa na mipango ya ufungaji migodi (yaani Mine Closure Plans) lakini mpaka sasa ni wamiliki wa migodi kumi (10) sawa na asilimia tano (5%) pekee ndiyo wamewasilisha mipango ya ufungaji wa migodi yao.

Aliongeza kuwa kati ya mipango yote kumi (10) iliyowasilishwa, mipango minne (4) tu sawa na asilimia 40 (40%) ndiyo ilikidhi vigezo na kuidhinishwa na Serikali na kuendelea kufafanua kuwa mpaka sasa ni migodi mitatu (3) tu sawa na asilimia 1.5 (1.5%) ndio imekwishaweka hati fungani zenye thamani ya dola za kimerekani milioni 41.

Alisema kuwa, ni takwa la sheria kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi mara uchimbaji unapoanza na kusisitiza kampuni zinazohusika na uchimbaji wa kati na mkubwa kuanza utekelezaji wake bila kuchelewa na kinyume chake, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayepuuza.

Aliongeza kuwa, sambamba na kutakiwa kuwa na  mipango ya ufungaji wa migodi, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ikisomwa na marekebisho yake ya mwaka 2017 na 2018, mbali na kutakiwa kuwasilisha mipango ya ufungaji migodi, ni wajibu wa kila mmiliki wa leseni kubwa za uchimbaji (yaani Mining License na Special Mining Licence) kuweka dhamana ya ukarabati mazingira ili iweze kutumika kurudishia mazingira yaliyoharibika ikitokea mgodi huo umefungwa ghafla au kutelekezwa bila kufanya ukarabati wa mazingira inavyotakiwa.

Alisisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuona wachimbaji wa madini nchini wakiendesha shughuli zao pasipo kuathiri mazingira huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini hivyo Sekta ya Madini kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akielezea mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini katika kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini nchini haziathiri mazingira, Biteko alieleza kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imekwishakamilisha Mwongozo wa Shughuli za Ufungaji Migodi (Mine Closure Guidelines) ambao utawarahisishia kuandaa na kutekeleza mpango wa ufungaji mgodi kama Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho yake inavyoelekeza.

Aliongeza kuwa, Serikali imejiimarisha kuhakikisha kuwa mazingira na jamii inayozunguka maeneo ya migodi hayaathiriki kutokana na shughuli za uchimbaji madini na kuendelea kusema kuwa Kurugenzi  ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira ya Tume ya Madini, imekuwa ikifuatilia kwa karibu masuala ya ufungaji migodi nchini ili kuhakikisha kuwa mazingira ya migodi hayatelekezwi bila kukarabatiwa baada ya shughuli za uchimbaji madini kumalizika; na Serikali haibebeshwi mzigo wa ukarabati mazingira ya migodi iliyotelekezwa.

Katika hatua nyingine Biteko alizitaka kampuni za madini nchini kutunza mazingira husuan mabwawa ya takasumu ili kuepusha athari za mazingira na afya za binadamu zinazoweza kutokea.

Alisema kuwa, uzoefu wa ukaguzi migodi nchini unaonesha kuwa kumekuwapo na uchafuzi mazingira kutokana na udhaifu wa usimamizi wa bwawa la takasumu ambao  umepelekea athari kubwa kwa usalama wa mazingira na afya za binadamu na wanyama katika maeneo ya uchimbaji.

Katika hatua nyingine Waziri Biteko alitoa rai kwa wamiliki wa migodi kusimamia vyema mabwawa ya kuhifadhi takasumu na kuongeza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya wamiliki migodi ambao hawasimamii vema mabwawa haya.

Aidha, aliwataka wamiliki wote wa migodi kushirikiana vyema na wakaguzi migodi wa Tume ya Madini tangu wakati wa kupanga wapi mabwawa haya yatajengwa, namna yatakavyojengwa na usimamizi wake wakati wote wa uchimbaji pamoja na kuwa na kibali cha kutumia mabwawa ya kuhifadhi takasumu kilichosainiwa kutoka Tume ya Madini. 

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula alizitaka kampuni za madini nchini kuwa na mipango ya utoaji wa huduma kwenye shughuli za uchimbaji wa madini (local content plan) pamoja na kuifuata.

Alisema kuwa, ni takwa la kisheria kwa kampuni za madini nchini kutumia huduma za ndani ya nchi ili kuhakikisha wananchi wanakuwa ni sehemu ya uchumi wa madini.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya mbali na kupongeza  wadau mbalimbali walioshiriki kwenye uandaaji wa kongamano husika alisema kuwa Tume ya Madini imejipanga katika kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alisema kuwa Tume ya Madini ipo tayari muda wote kuwasaidia wachimbaji wa madini ili uchimbaji wao uwe wenye manufaa kwao na taifa kwa ujumla.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals