[Latest Updates]: Kamati ya Bunge Yatembelea Soko la Madini Katoro

Tarehe : Sept. 24, 2019, 6:39 a.m.
left

Wafanyabiashara wa Madini katika Soko Dogo la Madini Katoro wameiomba Serikali iwaruhusu kuwa na Wasaidizi watakaowasaidia kununua madini maeneo  yenye mialo ya uchenjuaji na kuwauzia kwenye vituo vya ununuzi.

Wafanyabiashara hao wametoa ombi hilo wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilipotembelea  soko hilo  kwa lengo la kujifunza na kuangalia namna masoko ya madini yanavyoendeshwa.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Madini  Stanslaus Nyongo amesema kuwa, Sheria na Kanuni za biashara ya madini zinaelekeza kuwa shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini zinapaswa kufanyika  kwenye vituo  maalum vya manunuzi hivyo suala la kuwa na wasaidizi kwenye mialo wa kuwauzia wafanyabiashara hao linakinzana na Sheria ya Madini na Kanuni za madini kwenye masoko.

‘’   Kamati ndiyo inaishauri Serikali, ndiyo Bunge na Wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kutatua changamoto  tunazokutana nazo kwenye masoko. Sote tunajua Masoko ni Mapya, Sheria Mpya, Kanuni Mpya, hivyo tutaendelea  kutatua changamoto hizo yakiwemo masuala  ya vifaa na watumishi,’’ amesema Naibu Waziri  Nyongo.

Aidha, Naibu Waziri Nyongo amewataka wafanyabiashara wa madini na wachimbaji kuyatumia masoko ya madini  na kueleza kuwa, kufanya biashara ya madini nje ya masoko ni kujiweka kwenye matatizo. Pia, amewasisitiza  kuhusu matumizi sahihi na salama ya zebaki na kueleza kuwa, serikali itaendelea kuangalia njia mbadala za teknolojia ili kuweza kuachana na matumizi ya zebaki.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mariam Mzuzuri amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu wakati Serikali na Kamati zikiangalia namna ya kuzifanyia kazi   changamoto zilizowasilishwa kwao.

‘’ Kwa kuwa masoko haya yanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ni vyema suala hili mtuachie kwanza sisi na serikali ili tuliangalie,’’ amesema Mzuzuri. Kufuatia hali hiyo, Mzuzuri ameitaka wizara kuendelea kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na wachimbaji wa madini ili wajue namna ya kuyatumia masoko ya madini na kujua mwenendo mzima wa shughuli za madini na biashara ya madini inavyofanyika.

Katika hatua nyingine, kamati imeitaka Serikali kuhakikisha suala la Ulinzi kwenye masoko ya Madini halisubiri michakato bali linatakiwa kufanyiwa kazi haraka kutokana na rasilimali zilizopo katika masoko hayo.

Makamu Mwenyekiti amesema hayo kufuatia ombi la kuimarishwa kwa Ulinzi katika Soko la Katoro lililotolewa na Wafanyabiashara wa Madini sokoni hapo wakati  wa ziara yake mkoani Geita. 

Naye, Mjumbe wa Kamati hiyo Fred Mwakajoka ametaka taasisi zote za serikali zinazoshirikiana na Tume ya Madini kuendesha masoko hayo ziwepo katika masoko hayo ili kurahisisha utendaji wa majukumu ya masoko .

Baada ya kutembelea soko la Katoro, Kamati hiyo pia imetembelea Soko la Madini Kahama na baadaye  itatembelea  Nzega. Ziara ya kamati kutembelea masoko imefanywa na kamati hiyo baada ya kutembelea Soko Kuu la Madini Geita na Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals