[Latest Updates]: Mbibo Aomba Ushirikiano wa Teknolojia ya Madini Thailand

Tarehe : Feb. 22, 2024, 8:24 p.m.
left

Tanzania Yachungulia Fursa ya Makaa ya Mawe

Bangkok

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo ameiambia Serikali ya Thailand kuhusu uhitaji mkubwa wa Teknolojia za kisasa kwa ajili ya shughuli za madini nchini hivyo kuomba ushirikiano na nchi hiyo katika eneo hilo.

Nchi ya Thailand inatajwa kupiga hatua kubwa kwenye masuala ya teknolojia mbalimbali hususan zinazohusisha shughuli za uongezaji thamani madini jambo ambalo limepelekea nchi hiyo kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito vya thamani kubwa duniani huku bidhaa za mapambo zinazozalishwa kutoka viwanda mbalimbali vya nchi hiyo vikipata masoko kwenye nchi kubwa duniani.

Naibu Katibu Mkuu Mbibo ameeleza uhitaji huo alipokutana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Madini ya Thailand Bw.  Ekapat Wangsuwan ambapo ujumbe wa Tanzania umepata wasaa wa kupatiwa taarifa kuhusu Sekta ya Madini ya nchi hiyo.

‘’ Sisi tuna madini na ninyi mna teknolojia, tunaamini tukiunganisha nguvu katika eneo hili tutafika mbali na hili ni moja ya sababu kubwa kwanini tumefika hapa kuona namna tunavyoweza kushirikiana,’’
amesisitiza Mbibo.

Aidha, Mbibo amemueleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuhusu malengo ya ujumbe wa Tanzania kuwepo nchini humo ambayo pia yanahusisha kuendelea kujifunza kuhusu uendeshaji wa minada ya madini, kujenga mahusiano katika nyanja mbalimbali na ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho ya 69 ya Kimataifa ya Madini ya Vito.

Akizungumza katika mahojiano maalum baada ya ziara katika Wizara hiyo, Meneja Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini Bw. George Kaseza kasema, Tanzania ina fursa kubwa kwenye biashara ya Makaa ya Mawe kutokana na taarifa za nchi ya Thailand kuonesha mahitaji makubwa ya madini hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaagizwa nje.

Taarifa za takwimu za Wizara hiyo za mwaka 2022 zinaonesha Thailand ilitumia Dola za Marekani bilioni 3.6 kwa ajili ya uingizaji wa madini (mineral importation) nchini humo, ambapo sehemu kubwa ya madini hayo ikichangiwa na Makaa ya Mawe na Coke kwa zaidi ya asilimia 75. Nchi hiyo pia inaingiza kwa wingi madini aina ya Tin Ore, Dimension Stones na Kaolin ambayo yote yanapatikana nchini Tanzania.

‘’Kutokana na wasilisho lao, naona fursa kubwa kwa Tanzania  kwenye makaa ya mawe  kwasababu taarifa imeonesha kabisa  kwa kiasi kikubwa nchi hii inaagiza nje makaa ya mawe na sisi tunayo, tunaweza kunufaika na fursa hii na ni suala ambalo tunalichukua kwa uzito mkubwa,’’ amesema Kaseza.

Akizungumzia maendeleo ya Sekta ya Madini Thailand ukilinganisha na Tanzania, Kaseza amesema Tanzania inahitaji  kwa kiasi kikubwa kupata teknolojia za kisasa kama ilivyo Thailand  kwani katika maeneo mengine yanayohusu  uzalishaji na mauzo ya madini, bado Tanzania inafanya vizuri katika maeneo hayo na  kuongeza, pamoja na hayo bado tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa wenzetu,’’.

Katika taarifa ya Wizara hiyo imeonesha nchi hiyo ina aina 40 tu za madini yakihusisha ya viwandani, nishati, ujenzi, kilimo na teknolojia huku migodi iliyo hai ikiwa 495, wakati Tanzania ikiwa na aina za madini zaidi ya 100 na idadi kubwa zaidi ya migodi iliyopo hai ikilinganishwa na Thailand.

Aidha, kwa mwaka 2022 taarifa imeonesha kuwa thamani ya madini yaliyoyouzwa nje na Thailand ni Dola za Marekani milioni 616.17 zinazotokana na madini ya tin, gypsum na mengine. Kwa upande wa Tanzania mwaka 2022 madini yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 2.97 yaliuzwa nje ya nchi. Aidha, kwa Tanzania, takriban asilimia 80 ya mapato yanayotokana na madini yanatokana na mauzo ya dhahabu.

Katika ziara hiyo, Wizara ya Viwanda na Madini ya Thailand imefungua milango ya mazungumzo na ushirikiano kwa Tanzania na kuikaribisha kutosita kuendelea kupata taarifa za kina zinazohusu sekta hiyo.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals