[Latest Updates]: Miaka mitatu ya Dkt. Magufuli ilivyoboresha sekta ya madini

Tarehe : Dec. 31, 2018, 10:19 a.m.
left

Na Asteria Muhozya

Ni takriban Miaka Mitatu sasa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aingie madarakani kuliongoza Taifa la Tanzania katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Tangu Rais Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, Serikali anayoiongoza imefanya mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Madini kwa ajili ya kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinawanufaisha zaidi Watanzania.

Wanafunzi wa Shule za Sekondari jijini Arusha wakiangalia Madini ya Tanzanite wakati wa Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito na Usonara ya Arusha (AGF) yaliyofanyika Mwezi Mei,2017.[/caption]

Katika hatua za awali za kutekeleza mabadiliko hayo, Rais Magufuli Mwaka 2017, alianzisha Wizara mpya ya Madini baada ya kutenganishwa kwa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini kupitia Hati ya Majukumu (Instrument) Na.144 ya tarehe 22 Aprili, 2016 na Marekebisho yake ya tarehe 7 Oktoba, 2017.

Wizara hii ya Madini inaongozwa na Waziri wa Madini Angellah Kairuki na Naibu Mawaziri wawili, Stanslaus Nyongo na Doto Biteko pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila.

Mbali na uundwaji wa wizara hii mpya, yamefanyika mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, utungwaji wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za nchi wa Mwaka 2017, na Sheria ya Mamlaka ya nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili za nchi wa Mwaka 2017.

Utungwaji wa Sheria hizo mpya na mabadiliko ya Sheria ya Madini na Kanuni zake kumeboresha ulipaji wa mrabaha wa Serikali kutoka asilimia nne (4) na kuwa asilimia sita (6) ya bei ya madini ghafi kwa madini ya metali na vito na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini ya kiasi cha asilimia moja (1).

Mabadiliko haya pia yanaiwezesha Serikali kuwa na umiliki wa asilimia zisizopungua 16 za hisa huru kwenye Migodi mikubwa na ya kati, kodi ya zuio ya asilimia tano ya thamani ghafi ya madini imeanzishwa kwa wachimbaji wadogo.

Akizungumza katika kipindi Maalum cha TUNATEKELEZA, Waziri wa Madini Angellah Kairuki anasema, Serikali imeweza kufanya majadiliano na wamiliki wa migodi ya ACACIA na TANZANITE ONE ambapo majadiliano hayo yameleta matokeo chanya kwa Acacia kukubali kuilipa Serikali kiasi cha Dola za Marekani Milioni 300.

Katika maelezo yake, Waziri Kairuki anaongeza kuwa, baada ya majadiliano na Kampuni ya Tanzanite One wamekubali kulipa fidia pamoja na kodi watakayokubaliana kutokana na dosari zilizokuwepo hapo awali. “Tume maalum iliyoundwa na Rais inaendelea na majadiliano na makampuni yote makubwa yenye Mikataba na Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano, imedhamiria kuhakikisha rasilimali za madini zinasimimiwa ipasavyo ili ziweze kuchangia kwa ufanisi katika uchumi wa Taifa na ustawi wa Watanzania,” anasema Waziri Kairuki.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akiangalia bidhaa za mapambo zilizotokana na madini yanayopatikana nchini baada ya kuongezwa thamani.[/caption]

Aidha, Kairuki anaeleza kuwa, Mabadiliko ya Sheria yamewezesha na kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi ili madini yaongezewe thamani hapa nchini. Aidha, Waziri Kairuki anasisitiza, mabadiliko hayo yanaifanya migodi ilazimike kutumia bidhaa na huduma za ndani ya nchi na kutoa uwezo wa usimamizi kisheria wa Sekta ya Madini kutakakoleta ufanisi mkubwa.

Akisisitiza suala hili katika moja ya mikutano yake na wadau wa sekta ya madini nchini, Waziri Angellah Kairuki anasema Serikali imeweka ZUIO la kusafirisha madini ghafi nje ya nchi ikiwa na lengo la kuyaongezea thamani kabla ya kuyasafirisha. Katika kulisimamia hilo, anasema, Serikali kupitia Wizara ya Madini inaandaa Muswada wa Sheria ya uongezaji Thamani Madini, ili kuwezesha shughuli za Uongezaji Thamani madini kufanyika kwa kuzingatia Sheria na kusimamia vyema shughuli za uongezaji thamani madini nchini.

“Dhamira ya Serikali ni kujenga na kuendeleza Viwanda vya ndani, kuongeza Mapato ya Serikali kutoka Sekta ya Madini, na kurekebisha mapungufu yaliojitokeza katika utekelezaji wa Sheria zilizopo katika shughuli za uongezaji thamani madini hususani kwenye eneo la masonara,” anasisitiza Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki anaongeza kwamba, Wizara inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika shughuli za uongezaji thamani madini na kuendelea kutoa leseni za uchenjuaji na uyeyushaji wa madini ya metali. Pia, anafafanua kuwa, jumla ya maombi 27 ya uwekezaji kwenye smelters na refineries (ujenzi wa vinu (viwanda) vya uchenjuaji kwa ajili ya kusafisha na kuongeza thamani madini ya metali) yaliwasilishwa na uchambuzi unaendelea kufanyika ili kupata mwekezaji atakayekidhi vigezo.

Akizungumzia ukuaji wa Sekta ya madini katika Awamu hii anasema, Sekta ya Madini ilikua kwa asilimia 17.5 Mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 9.1 Mwaka 2015. Mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa uliongezeka na kufikia asilimia 4.8 Mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 4.0 Mwaka 2015.

Waziri Kairuki anasisitiza kuwa, Wizara imevuka malengo ya makusanyo ya maduhuli iliyopewa  mwaka 2017/18 ya Shilingi bilioni 194.66 na kuweza kukusanya Shilingi bilioni 298 sawa na asilimia 153.09.

Pia anaongeza, kuongezeka kwa kiwango cha ukuaji wa Sekta ya Madini kumetokana na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini; kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini; na usafirishaji wa madini nje ya nchi; kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 yaliyofanyika Mwaka 2017 na Kanuni zake.

Waziri wa Madini Angellah Kairuki akimsikiliza mmoja wa Wachimbaji wa Madini ya Bati katika moja ya ziara zake za kukagua shughuli za uchimbaji madini, Kyerwa mkoani Kagera.[/caption]

Akizungumzia uundwaji wa Tume ya Madini, ambayo ni zao la Mabadiliko ya Sheria ya Madini ya Mwaka, 2010, baada ya kufutwa kwa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (Tanzania Mineral Audit Agency –TMAA), Waziri Kairuki anasema kuundwa kwa Tume ya Madini, kumepelekea  usimamizi  wa karibu zaidi wa maeneo yenye uchimbaji wa madini. Aidha, uwepo wa ofisi za madini katika mikoa mbalimbali nchini unarahisisha ushughulikiaji wa maombi ya leseni, kupunguza migogoro na kuongeza makusanyo ya mrabaha.

“Pia, Tume imesimamia shughuli za uchimbaji ndani ya ukuta wa Mererani ili kudhibiti utoroshwaji wa Madini ya Tanzanites na madini mengine ili kuimarisha ukusanywaji wa kodi za Serikali,” anasema Waziri Kairuki.

Akizungumza katika Mkutano baina ya Waziri Kairuki na Wafanyabiashara wa Madini ya Tanzanite jijini Arusha, Mwenyekiti wa Chama Cha Wafanyabiashara wa Madini Tanzania (TAMIDA) Sam Mollel anasema ukuta uliojengwa kuzunguka migodi ya Tanzanite Mirerani umeongeza Imani kubwa kwa walaji wa madini hayo zikiwemo nchi za Marekani na Ulaya huku akisisitiza kuwa, ukuta wa Mirerani umedhibiti ajira za watoto migodini na kuondoa wizi wa vifaa migodini.

Haya ni baadhi tu ya mafanikio yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika Sekta ya Madini. Kwa hakika watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada hizi zinazofanywa na Serikali ambazo zinalenga kuhakikisha kwamba rasilimali madini zinalinufaisha taifa na watanzania wote.

Aidha, katika kuhakikisha kwamba sekta ya madini inachangia zaidi katika pato la Taifa na ukuaji wa uchumi, Waziri Kairuki anasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, lengo la wizara ni kuhakikisha Sekta ya Madini inachangia zaidi katika pato la Taifa ili hadi ifikapo mwaka 2025 sekta husika iweze kuchangia hadi kufikia asilimia kumi (10%).

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals