[Latest Updates]: Dkt. Biteko Aagiza Mradi wa Kabanga Nickel Kuanza Ulipaji wa Fidia kwa Wananchi

Tarehe : Sept. 30, 2022, 10:10 a.m.
left

Awataka wananchi kushirikiana na Mwekezaji.

Shilingi bilioni 30 zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia.

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameiagiza Kampuni ya Tembo Nickel inayomiliki mradi wa uchimbaji Madini ya Nikeli kulipa fidia wananchi watakaopisha eneo la mradi ambao uthaminishaji wa maeneo yao umekamilika. 

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo  alipotembelea mradi wa Kabanga Nikeli katika ziara iliyolenga kukagua hatua iliyofikiwa katika uendelezaji wa mradi husika katika eneo la Kabanga wilaya ya Ngara Mkoani Kagera.

Aidha, Dkt. Biteko amesema kuwa, zaidi ya Shilingi bilioni 30 tayari zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa Wananchi watakaopisha mradi huo. Pia, Amesisitiza taratibu za ulipaji fidia zianze ili Wananchi wasisubiri kwa muda mrefu na kupunguza tabia ya Wananchi wasio na nia njema kutegesha mazao kama migomba kwa ajili ya kufidiwa.

"Kama Serikali tunashauri na kuwaomba Wananchi tuachane na hizi tabia za ujanja ujanja ambapo watu wengi wanakuja hapa Tembo Nickel kupanda migomba kwa nia yake ni kutegesha ili alipwe fidia", amesema Dkt. Biteko. 

Vile vile, ametoa wito kwa Wananchi wa Ngara na Mkoa wa Kagera kutoa ushirikiano katika hatua zote muhimu ili kufanikisha ulipaji wa fidia katika maeneo hayo na uendelezaji wa mradi. 

Akizungumzia watu wanaochukua ardhi kwa ajili ya kulipwa fidia ya mali katika mradi huo amesema, tayari  maeneo yote ya mradi yalishachukuliwa picha za Satelite kuonesha hali ilivyokuwepo kabla na baada ya zoezi la uthaminishaji kuanza. 

Naye, Meneja Mkazi wa Kampuni ya Tembo Nickel Benedict Busunzu amesema kwa sasa baada ya kupata leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya Nikeli, Kampuni iko katika hatua za awali za kuhamisha Wananchi kutoka katika eneo la mradi ili kuanza ujenzi wa miundombinu ya mgodi. 

Ameongeza kuwa, baada ya kupokea maelekezo ya Waziri wa Madini kuhusu maeneo yaliyofanyiwa uthaminishaji, wananchi hao watapewa kipaumbele cha  kulipwa fidia zao. 

"Tunawaomba wananchi wa Ngara, wananchi wa Kagera kuonyesha ushirikiano maana mradi huu umesubiriwa kwa muda mrefu, vitu vidogo vidogo vinavyojitokeza tungependa tuvitatue kwa pamoja ili mradi usichelewe," Ameongeza. 

Ametoa mfano kwa wananchi wenye nyumba, mashamba pamoja na shule kuwa kwa mujibu wa Sheria yatatolewa fidia ili maeneo yote yafikiwe haraka na hatimaye mradi uanze. 

Kutokana na shughuli zinazofanyika kwa sasa katika eneo la mradi, Wananchi zaidi ya 200 wamepata ajira. Aidha, tayari mradi huo umelipa kodi kwa Serikali zaidi ya Shilingi bilioni 2.4 katika hatua za awali kabla ya kuanza uchimbaji rasmi. 

Katika ziara hiyo Dkt. Biteko ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adolf Ndunguru, Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Dkt. Musa Budeba, Kaimu Meneja wa Mazingira Tume ya Madini, Lucas Mlekwa na Kaimu Afisa Madini Mkazi, Samwel Shoo.

 

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals