[Latest Updates]: Waziri Mavunde Azindua Magari 25 ya Tume ya Madini

Tarehe : Oct. 21, 2024, 1:06 p.m.
left

Ni sehemu ya magari 89 na pikipiki 140 zinazotarajiwa kununuliwa

Lengo kuboresha Sekta ya Madini

Aagiza Magari kufungwa GPS

Ampongeza  Rais Samia kwa kuiongezea bajeti Wizara ya Madini 

DODOMA

Ikiwa ni mkakati wa kuimarisha usimamizi katika Sekta ya Madini hasa kwenye ukusanyaji wa maduhuli, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde amezindua magari mapya 25 kwa ajili ya kusambazwa kwenye Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa sambamba na kukabidhi magari hayo kwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa waliohudhuria uzinduzi huo.

Uzinduzi huo umehudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo na watendaji wengine kutoka Wizara ya Madini na Taasisi zake.

Akizungumza kwenye  uzinduzi huo, Mhe. Waziri Mavunde amesema kuwa Wizara imepanga kununua magari 89 na pikipiki 140 kama sehemu ya uboreshaji wa  usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa hasa kwenye  usimamizi wa ukusanyaji wa maduhuli na kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato na utoroshaji wa maduhuli.

Amesema kuwa, magari yaliyozinduliwa 25 ni awamu ya kwanza ya magari 89 yanayotarajiwa kuletwa sambamba na pikipiki 140 zitakazosambazwa kwenye ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa zilizopo nchi nzima.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele Sekta ya Madini kwa kuiongezea bajeti  Wizara ya Madini kutoka shilingi  bilioni 89 mwaka 2023/2024 hadi shilingi bilioni 231 katika mwaka wa fedha 2024/2025

“ Ongezeko  hili  ni dhahiri kabisa Dkt. Samia anatamani kuona Sekta ya Madini inaendelea kuimarika na mchango wake kuongezeka kwenye Pato la Taifa hasa kwenye ukusanyaji wa maduhuli, mathalan katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 tumepewa lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi Trilioni Moja ambapo ndani ya siku 90 tumeweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 287 ikiwa ni asilimia 106 ya lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 249 ndani ya kipindi husika,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Katika hatua nyingine, Mhe. Mavunde ameelekeza magari yote kufungwa GPS kwa ajili ya kuangalia mwenendo wake ili kuhakikisha yanatumika katika matumizi yaliyokusudiwa.

“Magari yote yatafungwa GPS ambapo Makao Makuu tutakuwa na uwezo wa kuona mwenendo wa magari kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini hasa kwenye shughuli za ukusanyaji wa maduhuli na ukaguzi wa migodi ya madini,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo amempongeza Waziri Mavunde kwa jitihada zake za usimamizi wa Sekta ya Madini na kuwataka watendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha wanaonesha matokeo chanya kwenye utendaji kazi.

Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo sambamba na kuishukuru Wizara ya Madini kwa magari husika amesema kuwa magari yatatumika kama chachu ya Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kwenye ongezeko la makusanyo ya maduhuli.

Amefafanua kuwa magari yote 85 yatakayonunuliwa yatagharimu zaidi ya shilingi bilioni 18.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals