Tarehe : May 7, 2018, 10 a.m.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ameipa siku saba kampuni inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited, kuwasilisha mikataba na nyaraka zote kati yake na kampuni ya Tanzania Gold Field Limited ili kubaini namna makubaliano ya mkataba yalivyofanyika ikiwa ni pamoja na ulipaji kodi serikalini.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe (kushoto) akielezea mchango wa sekta ya madini kwenye wilaya yake mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (kulia).
Biteko aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyasa kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania Limited na kutoridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo.
Waziri Biteko yupo katika ziara ya siku mbili mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua shughuli za madini pamoja na kuzungumza na wananchi na kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika shughuli za madini.
Alisema mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO Tanzania Limited, amebaini kuwa kampuni hiyo mara baada ya kukamilisha shughuli zake za utafiti wa madini ya dhahabu, kampuni hiyo iliikaribisha kampuni nyingine ijulikanayo kama Tanzania Gold Field Limited ya Canada kwa ajili ya kufanya shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la Magambasi wilayani Handeni mkoani Tanga pasipo kufuata taratibu za kisheria.
Aliendelea kusema kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field Limited iliwataka wachimbaji wadogo waliokuwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji madini katika eneo hilo kuondoka ili waanze uchimbaji madini jambo ambalo lilitekelezwa.
Alieleza kuwa, kampuni ya Tanzania Gold Field Limited ilianza shughuli zake bila kuwasilisha makubaliano ya kimaandishi kati yake na kampuni ya CANACO Tanzania Limited Serikalini pamoja na kodi jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.
Biteko aliendelea kusema kuwa kampuni inayotambulika mpaka sasa kisheria ni ya CANACO Tanzania Limited ambapo shughuli za madini katika eneo la Magambasi zimekuwa zikifanyika bila kufuata sheria na kanuni za mazingira.
Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko (katikati mbele) akiendelea na ziara katika eneo la kampuni inayojishughulisha na utafiti wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wilayani Handeni ya CANACO Tanzania Limited
“Haiwezekani wachimbaji wadogo ambao ndio wamiliki wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wakaondolewa halafu akapewa mwekezaji mkubwa ambaye mpaka sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya kuchejua mabaki wa udongo wenye dhahabu na kuuza na kuharibu mazingira huku wachimbaji wadogo wenye uwezo wa kuchimba dhahabu wakihangaika na kuishi katika lindi la umaskini,” alisema Biteko.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko alimtaka Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Handeni, Idrissa Yahya kuanza kazi mara moja ya uchambuzi wa vipengele vyote vya sheria na kanuni za madini ili kuangalia namna vilivyokiukwa na kuwasilisha ripoti ofisini kwake.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Wizara ya Madini ili kuimarisha sekta ya madini katika wilaya yake.
Imeandaliwa na:
Greyson Mwase, Tanga
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
5 Barabara ya Samora Machel,
S.L.P 2000,
11474 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
Barua Pepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.