[Latest Updates]: Maduhuli ya madini Chunya yazidi kupaa

Tarehe : Feb. 13, 2020, 9:20 a.m.
left

Hadi kufikia Januari 31 yafikia bilioni 24.1 sawa na lengo la asilimia 128 ya lengo la mwaka

Mwenyekiti Tume ya Madini apongeza Mkuu wa Wilaya, Afisa Madini Mkazi

Na Greyson Mwase, Chunya

Afisa  Madini Mkazi wa Mkoa wa Chunya, Godson Kamihanda ameeleza kuwa kuanzia kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 kilichoanza Julai, 2019 hadi Januari 31, 2020, ofisi yake imefanikiwa kukusanya jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 24.173 ikiwa ni sawa na asilimia 128 ya lengo la ofisi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambalo lilikuwa ni shilingi bilioni 18.861.

Kamihanda ameeleza hayo leo tarehe 13 Februari, 2020 kwenye ziara ya Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris  Kikula Wilayani Chunya mkoani Mbeya yenye lengo la kufuatilia maelekezo aliyoyatoa katika ziara yake aliyoifanya awali nchini kati ya  tarehe 29 Oktoba, 2019 na  tarehe 03 Novemba, 2019, kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wachimbaji wa madini.

Alisema kuwa maduhuli yamechangiwa na uanzishwaji wa Soko la Madini Chunya pamoja na vituo vidogo tisa vya ununuzi mdogo wa madini  vilivyopo katika maeneo ya Makongolosi, Matundasi, Itumbi, Chunya Mjini, Sangambi, Godima, Igundu na Shoga na vituo  vingine vilivyopo katika maeneo ya Mkwajuni na Saza katika Wilaya ya Songwe.

Aliongeza kuwa  ili kuhakikisha biashara ya madini inakuwa na  mchango mkubwa kwenye makusanyo ya maduhuli Chunya, kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ofisi yake ilitoa leseni 105 za ununuzi mdogo wa madini ya dhahabu kwa wale ambao walikubali kukaa katika vituo vidogo vya ununuzi wa madini.

Alisema pia ofisi yake ilitoa leseni 34 za ununuzi mkubwa wa madini katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2019 hadi Januari, 2020 tofauti na mwaka 2018/2019 ambapo ni leseni tisa tu zilitolewa.

Alisema kuwa,  kukua kwa biashara ya madini Chunya kumetokana na elimu ya  uhamasishaji ambayo imekuwa ikifanywa na Ofisi yake tangu kuzinduliwa kwa Soko la Madini Chunya mnamo tarehe 02 Mei, 2019 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila ikiwa ni siku tano baada ya Rais John Magufuli kutoa siku saba za kuhakikisha soko husika limefunguliwa.

Katika hatua nyingine,  Kamihanda aliongeza kuwa ili kuhakikisha usimamizi unaimarishwa kwenye vituo vya ununuzi wa madini, ofisi yake ilishirikisha viongozi wa kata ambao wamekuwa mstari wa mbele kusimamia biashara ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa zote kwa maafisa wa Tume ya Madini ambao wamekuwepo kwenye soko kuu la madini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi alisema kuwa Ofisi yake imekuwa ikisimamia kwa karibu sana suala la usalama kwenye biashara ya madini ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa madini.

Alisema kuwa, wananchi wameanza kuwa na uelewa mkubwa wa umuhimu wa kutumia masoko ya madini na kuwa walinzi wa rasilimali za madini huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Mbali na kupongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwenye Sekta ya Madini, alisema kuwa kabla ya maboresho kwenye Sekta ya Madini wachimbaji wa madini wasio waaminifu walikuwa wakitorosha madini hali iliyoikosesha Serikali mapato yake.

Wakati huo huo  Mwenyekiti wa Tume ya Madini alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhandisi Maryprisca Mahundi na  Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Chunya, Mhandisi Godson Kamihanda kwa usimamizi mzuri wa masoko ya madini hali iliyopelekea maduhuli ya Serikali kupaa.

Akielezea mikakati ya Tume ya Madini katika kuboresha huduma kwenye Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Profesa Kikula alisema Serikali imeongeza wataalam kwenye Ofisi za Madini, vitendea kazi ikiwa ni pamoja na magari na mashine za kupima madini kwenye masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Aidha, Profesa Kikula alifanya ziara katika vituo vya ununuzi wa madini vilivyopo katika eneo la Makongolosi na kuwataka wafanyabiashara wadogo kuwa wazalendo na waaminifu kwenye biashara ya madini huku wakilipa kodi mbalimbali Serikalini.

Pia Profesa Kikula alitembelea Kampuni za Uchenjuaji wa Dhahabu za PM na Otta Mining Limited   zilizopo katika eneo la Makongolosi na Kampuni ya Uchimbaji na Uchenjuaji wa Dhahabu ya Sunshine iliyopo katika eneo la Matundasi Wilayani Chunya Mkoani Mbeya.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals