Tarehe : July 20, 2018, 4:54 a.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko leo tarehe 19 Julai, 2018 amesema kuwa wanunuzi wa madini aina ya vito kote nchini wasiokuwa na mashine kwa ajili ya kukata na kung’arisha madini hayo watanyang’anywa leseni kwa kuwa wanaendesha biashara kinyume na taratibu kama Sheria ya Mpya ya Madini ya Mwaka 2017 inavyofafanua.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akiangalia madini aina ya vito kwenye mchanga kwenye eneo la uchenjuaji katika Mgodi wa Monica Gem uliopo Ngapa Mtoni wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo katika mkutano wake na wanunuzi wa madini aina ya vito kutoka Wilaya ya Tunduru uliofanyika mjini Tunduru mkoani Ruvuma ikiwa ni kama moja ya sehemu ya ziara yake katika mikoa ya kusini yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji madini zinazofanywa na wachimbaji wadogo, kuzungumza nao pamoja na kutatua changamoto mbalimbali.
Alisema kuwa ni kosa la kisheria kwa mnunuzi yoyote wa madini aina ya vito kuendesha biashara pasipo kuwa na mashine za kukatia na kung’arisha vito.
“Sheria inamtaka mnunuzi ambaye ni mtanzania kuwa na mashine 5 na mnunuzi wa kigeni kuwa na mashine 30 za kukata na kung’arisha madini ya vito, tunataka madini haya yaongeze thamani ndani ya nchi ili kuongeza mapato serikalini,” alisema Biteko.
Aidha, Biteko alimtaka Afisa Madini wa Tunduru Mjiolojia Abraham Nkya kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Zuberi Homera na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya Wilaya kufanya ukaguzi kwenye maduka ya wanunuzi watakaopewa leseni mpya ili kubaini kama wana mashine za kukata na kung’arisha vito na kuchukua hatua za kisheria kwa wanunuzi watakaobainika kutokuwa na mashine hizo ikiwa ni pamoja na kuwaandikia hati za makosa na kuwanyang’anya leseni.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliwataka wanunuzi wa kigeni wanaofanya biashara kwa ubia na watanzania kuhakikisha wanawashirikisha kwa kila jambo kama mikataba yao inavyotaka.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akifafanua jambo kwenye mkutano wake na wachimbaji wadogo uliofanyika katika kijiji cha Ngapa Mtoni wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Aliendelea kusema kuwa Sheria ya Madini inamtaka mzawa kuwa na umiliki wa isiyopungua asilimia 25 kwa kuwa hana uwezo wa kifedha na teknolojia na raia wa kigeni kuwa na asilimia 75 na kusisitiza kuwa ni vyema wakashirikiana kwa kila hatua kwenye biashara ya madini.
“Haiwezekani mbia wa Tanzania hatembelei kabisa eneo la biashara hali inayopelekea kutofahamu kabisa mwenendo wa biashara na kumwacha mbia ambaye ni raia wa kigeni akifanya kila kitu, hii inapelekea hata madini kutoroshwa nje ya nchi,” alisisitiza Biteko.
Aidha, aliwataka wanunuzi wa madini kuweka kumbukumbu za mauzo za kila siku ili kuweza kufanya ulinganisho wake na madini yanayosafirishwa nje ya nchi ili kujiridhisha na uwiano wake.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Biteko mbali na kutembelea baadhi ya migodi iliyopo katika kijiji cha Ngapa Mtoni kilichopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma alikutana na wachimbaji wadogo lengo likiwa ni kukusanya na kutatua kero mbambalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji hao wa madini ya vito, Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo wa Madini katika kijiji cha Ngapa Mtoni, Abel Kasibila alieleza changamoto hizo kuwa ni pamoja na kutumia nyenzo duni katika uchimbaji wa madini ya vito, kutokuwepo kwa watafiti ambao wangerahisisha kwenye ugunduzi wa madini na miundombinu ya barabara kutokuwa rafiki kwenye usafirishaji wa madini.
Alisema changamoto nyingine kuwa ni pamoja na malipo ya leseni kufanyika kwa fedha za kigeni na uwepo wa leseni kubwa bila ya wahusika kufahamika.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (katikati waliokaa mbele), Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Zuberi Homera (wa tatu kulia waliokaa mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wabunge na wachimbaji wa madini aina ya vito katika kijiji cha Ngapa Mtoni wilayani Tunduru mkoani Ruvuma
Awali akielezea hali ya uzalishaji wa madini ya vito na ujenzi katika wilaya ya Tunduru kwa mwaka wa fedha 2017/18, Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Zuberi Homera alisema takwimu za usafirishaji wa madini ya vito katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni, 2018 zilionyesha kuwa jumla ya gramu 24,279.416 zenye thamani ya Dola za Marekani 108, 807 zilisafirishwa na kulipiwa mrabaha wa shilingi milioni 14.6.
Aliongeza kuwa jumla ya gramu 1196.01 zenye thamani ya shilingi milioni 160.9 zilizalishwa na kulipiwa mrabaha wa awali wa shilingi milioni 9.6 katika Ofisi ya Madini Tunduru.
Aliendelea kufafanua kuwa jumla ya tani 1,882 za madini ya ujenzi (mchanga) zenye thamani ya shilingi milioni 33.9 zilizalishwa na kulipiwa mrabaha wa shilingi milioni 1,050,000.
Aidha alisema kuwa wilaya ya Tunduru ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 85.1 kati ya shilingi milioni 100 iliyopangiwa kukusanya kwa mwaka 2017/2018 sawa na asilimia 85.16.
Akielezea mikakati ya ukusanyaji wa maduhuli, Homera alisema kuwa wilaya yake imepanga kutoa huduma za ugani kwa kutoa ushauri kwa wachimbaji wadogo wa madini kuhusu uchimbaji bora, salama na unaozingatia utunzaji wa mazingira na kuishauri Wizara ya Madini kutoa mafunzo kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Wakala wa Utafiti wa Madini na Jiolojia Tanzania (GST) kwa wachimbaji wadogo na viongozi wa Serikali kwenye maeneo yenye madini ili waweze kuelewa Sheria Mpya ya Madini na kanuni zake.
Aliitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuiomba Tume ya Madini kutenga eneo la Ngapa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini katika wilaya ya Tunduru, kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya machimbo na kuhamasisha wenye uwezo kuanzisha viwanda vya kusanifu madini ya vito.
Imeandaliwa na:
Greyson Mwase, Tunduru
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
Kikuyu Avenue,
P.O Box 422,
40474 Dodoma,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
BaruaPepe: info@madini.go.tz,
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.