[Latest Updates]: Nyongo, Biteko wapongeza JKT ujenzi wa ukuta Mererani

Tarehe : April 28, 2018, 11:55 a.m.
left

  • Wawataka Watanzania kuondoa hofu kuhusu manufaa yake
  • Ujenzi wafikia asilimia 98

Naibu Mawaziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Dotto Biteko wamefanya ziara mahali kunapojengwa ukuta maalum kuzunguka machimbo ya Tanzanite Mererani na kutoa pongezi kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kutekeleza shughuli ya ujenzi kwa kasi na kiwango cha hali ya juu.

Naibu Mawaziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) na Stanslaus Nyongo (katikati) wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (kulia), walipomtembelea ofisini kwake Jumatatu Februari 12 mwaka huu kabla ya kutembelea Mererani kunapojengwa Ukuta unaozunguka Machimbo ya Tanzanite kwa ajili ya kukagua maendeleo yake.[/caption]

Wakizungumza kila mmoja kwa wakati wake, baada ya kuhitimisha ziara yao katika eneo hilo, Jumatatu Februari 12 mwaka huu, Naibu Mawaziri hao walisema iko haja kwa watanzania wote kuiga uzalendo uliooneshwa na wanajeshi hao.

“Mfano tuliouona kutoka JKT kutokana na uzalendo wao ni fundisho kwa wananchi wote. Vijana wa JKT wamefanya kazi kubwa. Tumeshuhudia ari yao kubwa ya kufanya kazi kwa kujitolea. Uzalendo waliouonesha ni mfano wa kuigwa na watanzania wote,” alisema Nyongo.

Aliongeza kuwa wametembelea na kujionea wenyewe kazi ya ujenzi inavyoendelea na kuridhika. Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa, Ukuta ulikuwa ujengwe ndani ya miezi sita lakini katika muda wa miezi mitatu, uko katika hatua za mwisho kukamilika, jambo ambalo linapaswa kupongezwa na mpenda maendeleo yeyote.

Aidha, Naibu Mawaziri walipongeza jitihada zilizofanywa na Jeshi hilo chini ya usimamizi wa Kamanda wa Operesheni Ujenzi wa Ukuta Mererani, Kanali Charles Mbuge, ambazo zimesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za ujenzi.

“SUMA-JKT wametupa somo kubwa sana watanzania, kwamba utumiaji wa wakandarasi wanaopandisha bei hauisaidii nchi. Na katika hili, nina uhakika baada ya muda watu watatoka mataifa mengine kuja kujifunza hapa kwetu,” alisisitiza Naibu Waziri Biteko.

Kuhusu suala la Ujenzi wa Ukuta husika kuhofiwa na baadhi ya watu kuwa utaondoa au kupunguza fursa za wananchi kunufaishwa na madini hayo adhimu, Naibu Mawaziri kwa umoja wao waliwataka watanzania kuondoa hofu kwani lengo hasa la ujenzi huo ni kuongeza fursa kwa watanzania na Taifa kwa ujumla kunufaika na siyo kinyume chake.

“Niwahakikishie wananchi wa Simanjiro na Tanzania yote kwa ujumla, kuwa Ukuta huu unakwenda kudhibiti rasilimali yao ya madini ya tanzanite ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikinufaisha mataifa mengine wakati inapatikana Tanzania pekee,” alisema Biteko.

Matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Naibu Mawaziri wa Madini, Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ukuta unaozunguka Machimbo ya Tanzanite Mererani, Februari 12 mwaka huu.[/caption]

Aliwaomba wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kuhakikisha rasilimali hiyo inalinufaisha Taifa ipasavyo.

Pamoja na pongezi hizo kwa JKT, Nyongo na Biteko pia walitoa pongezi kwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuasisi suala la ujenzi wa Ukuta huo.

“Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuhakikisha Ukuta huu unajengwa kutokana na maagizo yake aliyoyatoa Septemba 20 mwaka jana ambayo yalipelekea JKT kuanza utekelezaji wa awali mara moja siku moja baadaye yaani Septemba 21,” alisema Nyongo.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa hivi sasa ujenzi umekamilika katika eneo lote lenye urefu wa kilometa 24.5 na kwamba hatua iliyofikiwa sasa ni kukamilisha mambo madogo madogo yanayolenga kuimarisha zaidi Ukuta huo.

Aidha, Nyongo aliongeza kuwa kazi iliyobaki kwa Wizara ya Madini ni kuhakikisha inafungwa mitambo ya kisasa ya ulinzi ili eneo liwe na usalama zaidi. “Vilevile tunataka hili Geti likianza kufanya kazi tuwakague wanaoingia na kutoka wanaingia na nini na kutoka na nini. Lengo ni kuimarisha zaidi ulinzi na kulinda rasilimali yetu ya tanzanite.”

Suala jingine ambalo Naibu Mawaziri hao walieleza ni kuhusu utoaji wa elimu kwa wananchi ili wajue utaratibu watakaoutumia kuendesha shughuli zao za madini ndani ya ngome ya Ukuta huo.

Walisema kuwa, kwa Kampuni zinazoendesha shughuli zake mahala hapo, zitashirikishwa pia ili kuangalia namna watakavyotunza Ukuta huo lakini pia ni kwa namna gani Ukuta huo utumike kulinda shughuli zote za uchimbaji wa madini.

Matukio mbalimbali wakati wa ziara ya Naibu Mawaziri wa Madini, Dotto Biteko na Stanslaus Nyongo kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ukuta unaozunguka Machimbo ya Tanzanite Mererani, Februari 12 mwaka huu.[/caption]

Kwa upande wake, Mbunge wa Simanjiro James Millya, ambaye alishiriki katika ziara hiyo, aliishukuru na kuipongeza Serikali kwa kupigania maslahi ya wananchi wa Jimbo lake kwa kuhakikisha Ukuta huo unajengwa ili kudhibiti utoroshwaji wa madini ya tanzanite.

Naye Kanali Mbuge alitoa rai kwa Taasisi mbalimbali za Serikali kuendelea kuwapatia kazi mbalimbali JKT kutokana na mfano mzuri waliouonesha kupitia ujenzi wa Ukuta husika.

“Kupitia ujenzi wa Ukuta huu, naomba tupewe kazi nyingi. Nadhani mfano wa utendaji kazi wetu unaozingatia uzalendo wa hali ya juu tumeuonesha. Hapa kazi tu, hakuna maneno,” alisisitiza Kanali Mbuge.

Akitoa mfano, Mbuge alieleza kuwa, moja ya eneo ambalo JKT imefanikiwa kuokoa fedha na kupunguza gharama za ujenzi wa Ukuta ni kutokana na kuwatumia vijana wa JKT ambao walijitolea kufanya kazi hiyo bure pasipo malipo yoyote. “Tungesema tuwalipe vijana hawa, basi tungeongeza gharama ya shilingi bilioni 2.6.”

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula mbali na kupongeza kazi iliyofanyika, alisema kuwa wamejipanga, kuanzia Februari 15 mwaka huu kuimarisha zaidi ulinzi wakati wakisubiri ufungwaji wa vifaa vya kisasa vya ulinzi katika Ukuta.

“Simaanishi kwamba kwa sasa hakuna ulinzi, la hasha, ulinzi upo isipokuwa tunaimarisha zaidi. Hii itahusisha ukaguzi madhubuti wa kila anayeingia na kutoka, hata kabla hatujafunga vifaa vya kisasa vya ulinzi zikiwemo Kamera za CCTV.”

Jumla kuu ya gharama za ujenzi wa Ukuta wa Mererani ni shilingi bilioni 5.6 ambapo kwa mujibu wa Kanali Mbuge, ujenzi umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilishwa mapema zaidi kabla ya muda alioutoa Rais.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba, Mererani

Afisa Habari,

Wizara ya Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@madini.go.tz,                                             

Tovuti: madini.go.tz

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals