Tarehe : Oct. 6, 2018, 8:01 a.m.
Na Greyson Mwase, Dodoma
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa siku mbili kwa kampuni inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya vito katika kijiji cha Kwahemu Wilayani Chamwino mkoani Dodoma ya Ruvu Gemstone Mining Co. Limited inayomilikiwa na Kimon Dimitri kuwasilisha ofisini kwake ripoti ya utekelezaji wa mpango wa utoaji wa huduma kwa jamii kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kutoa maamuzi ya serikali.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) akiangalia moja ya mawe yanayochongwa na Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga katika eneo la Itiso lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma katika ziara yake ya siku moja katika machimbo yaliyopo katika Wilaya ya Chamwino yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali kwenye shughuli za uchimbaji madini tarehe 06 Oktoba, 2018.[/caption]
Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo jana tarehe 06 Oktoba, 2018 alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kwahemu kilichopo Wilayani Chamwino mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja katika Wilaya ya Chamwino yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini pamoja na wananchi wanaozunguka migodi.
Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, Mbunge wa Jimbo la Chinolwa, Joel Makanyaga, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Dodoma, Joshua Nduche, vyombo vya ulinzi na usalama vya Wilaya pamoja na waandishi wa habari.
Alisema kuwa, haiwezekani kampuni inayoendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya vito ya Ruvu Gemstone Mining Co. Limited ikaendesha shughuli zake pasipo kunufaisha wananchi wanaozunguka migodi yake.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali kamwe haitamvumilia mwekezaji wa aina yoyote atakayeendesha shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini kwa kukiuka Sheria Mpya ya Madini yenye kipengele kinachowataka wawekezaji kuchangia katika uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya, miundombinu ya barabara na shule.
“Serikali kupitia Wizara ya Madini imejipanga katika kuhakikisha watanzania wote wananufaika na uwepo wa rasilimali za madini kupitia kodi, tozo mbalimbali pamoja na mpango wa utoaji wa huduma za jamii,” alisema Naibu Waziri Nyongo.
Moja ya mitambo ya kukata mawe katika Mgodi wa Mawe unaomilikiwa na Sisti Mganga katika eneo la Itiso lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma[/caption]
Alisisitiza kuwa, ni lazima nakala za ripoti zisambazwe kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Diwani na Mbunge ili kubaini ukweli wa madai ya mwekezaji kuwa amekuwa akichangia katika huduma za jamii tangu alipoanza kuchimba madini ya vito mwaka 1986.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo alimtaka mwekezaji kuhakikisha anadumisha mahusiano na jamii inayozunguka mgodi ili kuepusha migogoro inayotokea mara kwa mara.
Awali wakiwasilisha kero kwa Naibu Waziri Nyongo wananchi wa kijiji hicho walimweleza kuwa tangu kuanzishwa kwa mgodi husika hawajaona manufaa ya aina yoyote zaidi ya kunyanyaswa kwa kunyang’anywa ardhi, kupigwa na wakati mwingine kufungwa jela.
Akiwasilisha kero kwa niaba ya wananchi hao, Daudi Kiloka ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kwahemu alisema kuwa awali walikuwa na shamba kubwa lenye ukubwa wa takribani heka 500 chini ya Umoja wa Bega kwa Bega wa kijiji hicho lakini baadaye shamba hilo lilikuja kutwaliwa na mwekezaji huyo.
Aliendelea kusema kuwa, wananchi wamekuwa wakikosa huduma muhimu ikiwa ni pamoja na shule, maji na vituo vya afya hali inayolazimu wananchi wengi kutumia muda mwingi kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.