[Latest Updates]: Nyongo Ataka Watumishi Madini Kuepuka Rushwa

Tarehe : Feb. 18, 2019, 1:32 p.m.
left

Na Asteria Muhozya, Dodoma

Naibu wa Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amewataka watumishi wa Wizara ya Madini kujiepusha na vitendo vya rushwa ikiwemo kuzuia rushwa katika sehemu zao za kazi kwani suala hilo linasababisha migogoro kwenye sekta ya madini.

Naibu Waziri Nyongo aliyasema hayo Februari 13 wakati akifungua mkutano wa Baraza la wafanyakazi la wizara na kuongeza kuwa, serikali inafuatilia mienendo ya watumishi wa sekta husika.

Alisema kuwa, wako watumishi wanaomiliki leseni kwa dhuluma suala ambalo pia limechangia kuwepo kwa migogoro mingi kwenye sekta na kueleza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Magufuli anasisitiza suala la kuzingatia maadili katika utumishi wa umma na hususan katika sekta ya madini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo alilitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhakikisha linajiendesha kwa faida na kusisitiza kuwa Serikali inataka gawio.

Aidha, aliutaka uongozi wa STAMICO kuzingatia maslahi ya watumishi kwa kutoa motisha mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo lengo likiwa ni kuboresha utendaji kazi wa shirika kwa ujumla.

Akizungumzia mafanikio makubwa katika Sekta ya Madini, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa ni pamoja na mabadiliko ya Sheria ya Madini na kusisitiza kuwa kwa Afrika Tanzania imekuwa mfano kama nchi bora inayosimamia vyema rasilimali za madini.

“Sifa bora kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini zisitufanye tubweteke bali tuendelee kufanya kazi kwa ubunifu wa hali ya juu huku tukizingatia maadili ya kazi,” alisema Nyongo

Nyongo aliendelea kusema kuwa, kama moja ya mikakati ya kutoa motisha kwa watumishi, uongozi wa Wizara unatakiwa kutoa fursa mbalimbali kwa watumishi ikiwa ni pamoja na mafunzo.

Wakati huo huo, akizungumza kwa niaba ya watumishi, Mwakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Tawi la Wizara ya Madini, Joyce Manyama alisema kuwa watumishi kupitia chama chao watafanya kazi bega kwa bega na uongozi wa Wizara ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na viwanda vingi vya uongezaji thamani madini ili kufikia malengo ya Serikali kupitia mchango wa Sekta ya Madini kwenye ukuaji wa Pato la Taifa.

Aidha, Manyama alichukua fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Shirika la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Nchini (FEMATA), wachimbaji wadogo kwa kuitisha mkutano uliofanyika hivi karibuni baina yao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli

Vilevile, aliishukuru Wizara kwa kuanzisha mfumo mpya wa utunzaji wa kumbukumbu za Wizara unaojulikana kama Electronic Filing Management System ambao utaboresha utunzaji wa kumbukumbu na kurahisisha upatikanaji wake pindi zinapohitajika.

Pia, aliiomba Wizara kuendelea kusimamia zoezi la upandishwaji wa vyeo ili watumishi waweze kupandishwa vyeo kulingana na sifa wanazokuwa nazo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila alisema kuwa Wizara itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kazi ili kila mtumishi afanye kazi kwa ubunifu zaidi.

Aliongeza kuwa, kwa sasa Wizara inafanya vizuri ambapo Sekta ya Madini imekua kwa asilimia 18 huku mchango wa sekta kwa fedha za kigeni ikiwa ya tatu nyuma ya Kilimo na Utalii na kueleza kwamba, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna rushwa na kukosekana uadilifu.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals