Tarehe : July 24, 2018, 5:03 a.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko amewataka wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini kwa njia ya ujanja ikiwa ni pamoja na kukwepa kulipa kodi serikalini, kutafuta kazi nyingine kwani Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Madini imejipanga kudhiti biashara haramu ya madini.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa (kulia) kabla ya kuanza ziara ya kikazi katika mkoa Mtwara tarehe 21 Julai, 2018.
Naibu Waziri Biteko aliyasema hayo leo tarehe 21 Julai, 2018 kwenye mkutano wake na wazalishaji wa chumvi, wachimbaji madini ya jasi pamoja na wawakilishi kutoka kampuni ya saruji ya Dangote uliofanyika mjini Mtwara wenye lengo la kufuatilia maelekezo aliyoyatoa katika kikao kilichofanyika mapema tarehe 19 Januari, 2018, kubaini changamoto kwenye shughuli za madini pamoja na kuzitatua.
Alisema kuwa Wizara ya Madini imejipanga katika kudhibiti mianya yote ya ukwepaji kodi, utoroshaji wa madini na rushwa ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Akielezea mikakati ya Serikali katika kuboresha shughuli za wachimbaji wa madini ya chumvi Biteko alisema kuwa, Serikali imeondoa kodi zote zisizo za lazima ili wachimbaji wadogo wapate faida zaidi na kulipa kodi stahiki serikalini.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Biteko aliagiza wachimbaji madini hao kuhakikisha wanalipa kodi stahiki ya madini mara baada ya kufanyika kwa mauzo kwenye kituo cha mwisho (gross value) badala ya mauzo ya hapo hapo mgodini (net back value).
“Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kifungu cha 87 (6) kinaeleza kuwa kodi ya madini itakokotolewa baada ya bei ya mwisho nje ya nchi kule yanapouzwa madini hayo na si mgodini,” alieleza Biteko.
Aliendela kusema kuwa wakati wa kufanya biashara ya madini kwa ufanisi ni sasa kwani hakuna urasimu na ujanja serikalini, hivyo kupelekea leseni za madini kutolewa kwa wakati na kusisitiza kuwa kinachohitajika kwa wachimbaji wadogo ni kufuata sheria na kanuni za uchimbaji madini.
Wakati huo huo wachimbaji wadogo wa madini katika mikoa ya Lindi na Mtwara walimpongeza Naibu Waziri Biteko kwa kutatua changamoto zilizokuwa zinawakabili kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 kwa muda mfupi tu wa miezi sita tu.
“Mheshimiwa Naibu Waziri tunashukuru mno kwani tangu ulipokutana na sisi mapema Januari 19, mwaka huu mjini Mtwara na kutoa maelekezo kwa watendaji na kufuatilia maelekezo yako, changamoto zote zimeisha ndani ya miezi sita, tuaendelea kuunga mkono juhudi zako za kuboresha sekta ya madini kupitia wachimbaji wadogo,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Lindi (LIREMA), Peter Ludovick kupitia taarifa yake kwa Naibu Waziri Biteko.
Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko (kushoto) akizungumza na wachimbaji wa madini ya jasi, wazalishaji wa chumvi pamoja na wawakilishi kutoka kampuni ya saruji ya Dangote.
Akielezea pongezi hizo, Biteko alisema yeye hastahili pongezi hizo bali ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa yeye ndiye aliyeelekeza Wizara ya Madini kuwaondolea wachimbaji kero.
Aliendelea kusema kuwa anayestahili kupongezwa ni Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ambaye ndiye msimamizi mkuu wa Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Fedha kwa kukubali kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Fedha na kusisitiza kuwa hao ndio wanaostahili pongezi na sio yeye.
Wakati huohuo, Biteko alikutana na watumishi wa Ofisi ya Madini Mtwara na kuwataka kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa huku akiahidi kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji kazi.
Imeandaliwa na:
Greyson Mwase
Afisa Habari,
Wizara ya Madini,
Kikuyu Avenue,
P.O Box 422,
40474 Dodoma,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,
BaruaPepe: info@madini.go.tz,
Tovuti: madini.go.tz
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.