[Latest Updates]: GST Yaishawishi Slovakia Kuwekeza Sekta ya Madini Tanzania

Tarehe : Nov. 10, 2021, 8:33 a.m.
left

Asteria Muhozya na Abubakari Kafumba, UAE

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba ameishawishi nchi ya Slovakia kuwekeza Tanzania kwenye uchimbaji au ununuzi wa Madini ya Viwandani yanayotumika katika kutengeneza vifaa vya teknolojia mbalimbali yakiwemo magari.

Dkt. Budeba alimweleza Mkurugenzi wa Uchumi na Uwekezaji wa Kampuni ya Sario inayomilikiwa na Serikali ya nchi hiyo Bw. Egon Zorad, kuhusu uwepo madini hayo ambayo ni malighafi katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za teknolojia.

 ‘’Tumeona Slovakia imepiga hatua katika masuala ya teknolojia ambapo wanatengeneza magari yanayotumia haidrojeni na tumeona wametengeneza mifano ya ndege. Kwetu sisi kama sekta ni fursa kuwavutia waje kuwekeza kwetu kwa ajili ya kupata malighafi ya kutengeneza bidhaa zao kwa sababu vitu vyote tulivyoviona vinahitaji malighafi zinazotokana na madini kama nickel, copper, rare earth elements, graphite na mengine ambayo yote yapo kwetu,’’ alisema Dkt. Budeba.

Alitoa kauli hiyo wakati wa kikao na mwakilishi huyo aliyefika katika banda la Tanzania baada ya wataalam wa Tanzania kutembelea banda la nchi hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Expo 2020 Dubai, ambapo walipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali zinazozalishwa na nchi ya Slovakia likiwemo gari linalotumia hydrojeni.

Kwa mujibu wa Zorad, gari hilo limetengenezwa kwa takriban miaka mitatu na waundaji wake wakihusisha wataalam kutoka Vyuo Vikuu vya nchini humo kwa kushirikiana na Serikali na kampuni binafsi. Wataalam wa watanzania baada ya kutembelea banda hilo walifahamishwa kuhusu namna nchi hiyo inavyojaribu kukuza teknolojia zake na kuhamia katika mifumo mingine ya kiteknolojia ikiwemo matumizi ya magari yanayotumia umeme.

Aidha, Dkt. Budeba alimuhakikishia mwakilishi huyo kuhusu upatikanaji wa rasilimali za kutosha yakiwemo mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara yaliyopo nchini ikiwemo hali ya usalama, na uwepo wa miundombinu ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu huku pia, akieleza nia ya Tanzania kuunganishwa na wawekezaji wengine wakubwa kutoka Slovakia.

Pia, mbali na kuchimba na kununua madini, Dkt. Budeba aliishawishi nchi hiyo kufikiria namna inavyoweza kuanzisha kampuni ya uundaji magari nchini Tanzania kutokana na uhakika wa upatikanaji wa malighafi ambazo zitahitajika katika uundaji bidhaa hizo. Vilevile, Dkt. Budeba alimuhakikishia kuwa, tayari Tanzania inayo kanzidata yenye taarifa za kutosha kuhusu uwepo wa madini mbalimbali ya viwandani na teknolojia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Sario, Bw. Zorad alishukuru kukutana na Wizara ikiwemo kufahamishwa kuhusu uwepo wa rasilimali madini na hivyo kutaka kupatiwa taarifa za kutosha kuhusu masuala muhimu ya uwekezaji na biashara ya madini Tanzania ili pia kampuni hiyo iweze kuiunganisha Tanzania na kampuni nyingine zilizoko  nchini Slovakia.

‘’Nataka sana Tanzania kuwa moja ya nchi tutakayoshirikiana nayo kwenye biashara na vyuo vyetu. Tumeelezwa kuwa nchi yenu iko kwenye nafasi nzuri kibiashara katika masuala ya madini. Slovakia tunaandaa mkutano wa wawekezaji na tunatarajia kualika angalau nchi moja kutoka Afrika na haina shaka itakuwa Tanzania,’’ amesema Zorad.

Mbali na masuala yanayohusu madini, pia, mwakilishi huyo wa Kampuni ya Sario, alieleza nia ya Slovakia kutaka ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania hususan kwenye masuala ya tafiti.

Katika hatua nyingine, Dkt. Budeba na Maafisa wengine wa Wizara ya Madini na taasisi zake walifanya mkutano kwa njia ya mtandao na mwekezaji kutoka China aliyetaka kuwekeza kwa kushirikiana Shirika la Madini la Taifa (STAMICO). Aidha Dkt. Budeba alimuunganisha mwekezaji huyo na Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO kwa hatua zaidi.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Banda la Tanzania kwenye Maonesha ya Kimataifa ya Expo 2020 Dubai, Getrude Ng’weshemi kutoka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) ameendelea kusisitiza ushiriki wa uhakika kama huo kwa sekta nyingine ambazo zinatarajiwa kushiriki katika maonesho haya ili kuhakikisha Tanzania inatumia vilivyo fursa zilizopo Dubai na kwingineko duniani kupitia maonesho haya.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals