[Latest Updates]: Sekta ya uchimbaji mdogo wa madini haijaachwa nyuma-Mhandisi Mulabwa

Tarehe : Oct. 8, 2019, 7:10 a.m.
left

Kamishna wa Madini nchini, Mhandisi David Mulabwa amesema, Serikali ya Tanzania inatambua uwepo na umuhimu wa wachimbaji wadogo wa madini nchini na hivyo kutekeleza sera inayotaka sekta hiyo kusimamiwa kikamilifu na kuleta tija.

Ameyasema hayo leo tarehe 08 Oktoba, 2019 alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Kanda wa Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Sekta za Madini na Viwanda wenye dhima inayosema “Kuongeza uelewa kwa wafanyakazi juu ya Dira ya Madini kwa Afrika” (Deepening workers understanding of the African Mining Vision).

Mkutano huu utafanyika kwa siku mbili ukijumuisha nchi zilizopo Chini ya Jangwa la Sahara ambapo Tanzania ni mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika katika hoteli ya White Sand jijini Dar es Salaam.

Akijibu swali la mmoja wa wajumbe wa mkutano huo kutoka nchini Ghana, Mhandisi Mulabwa alisema Serikali kupitia Wizara ya Madini inatekeleza mipango mbalimbali katika kuhakikisha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini inakua na kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia jitihada hizo, Mhandisi Mulabwa alisema ni pamoja na kurasimisha sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ili kuiwezesha serikali kuwahudumia wachimbaji hao kwa ukaribu mkubwa.

Pamoja na kurasimisha shughuli hizo Mhandisi Mulabwa alisema Serikali inatoa elimu kwa wachimbaji wadogo katika maeneo ya usalama, mazingira na afya ili kuwawezesha wachimbaji hao kufanya kazi zao katika mazingira salama na hivyo kuepusha ajali zisizokuwa za lazima na hivyo kutunza nguvu kazi.

Aliongeza kuwa, Serikali imejenga vituo vya mfano saba (7) nchi nzima vikiwa na lengo la kuonesha namna bora ya  uchimbaji na uchenjuaji wa madini ya dhahabu pasipo kutumia mercury ambayo ina madhara makubwa kwa watumiaji na jamii kwa ujumla.

Pamoja na vituo hivyo, Serikali inafanya juhudi kubwa ya kuwaunganisha wachimbaji wadogo na taasisi za kifedha na mabenki ili kuwawezesha kupata mikopo na kuwekeza katika shughuli za uchimbaji.

Aidha, Mhandisi Mulabwa alisema, Sheria za kazi zinasimamiwa ipasavyo katika sekta ya madini na kueleza kuwa endapo mfanyakazi yeyote katika sekta hiyo amepatikana na udhahifu akiwa kazini taratibu na kisheria zinafuata mkondo wake na endapo itabainika mtumishi anahitajika kulipwa fidia, atalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

Mhandisi Mulabwa alitumia fursa hiyo kuwaalika wadau wote wa madini walioshiriki katika mkutano huo kuja kuwekeza nchini huku akieleza kuwa fursa na maeneo kwa ajili ya uwekezaji katika seka ya madini ipo.

Amesema serikali kupitia Tume ya Madini inaendelea kupokea maombi ya leseni na kutoa leseni kwa wadau watakaoonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini.

“Maeneo ya uwekezaji yametengwa, na maeneo yamelenga uwekezaji mkubwa na mdogo wa madini, hivyo yeyote mwenye nia ya kuwekeza anakaribishwa” alisisitiza.

Akihitimisha hotuba yake Mhandisi Mulabwa, aliwataka wadau hao kuelewa kuwa Tanzania haipo nyuma katika kusimamia dira ya madini ya Afrika ya kuhakikisha rasilimali madini inawanufaisha waafrika kwa manufaa ya bara Afrika kwa ujumla

Amewahakikishia wadau wote wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya madini nchini kuwa serikali ya Tanzania itawapa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha wanapata fursa ya kuwekeza nchini kwa wakati.

Aidha, amesema serikali ipo tayari kufanya kazi na Shirikisho hilo ili kuhakikisha malengo ya kuanzisha shirikisho hilo la kuhakikisha inawasaidia wafanyakazi kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao linafikiwa.

Akizungumza baada ya kumaliza awamu ya kwanza ya mkutano huo Katibu Mkuu msaidizi wa Shirikisho hilo kutoka nchini Uswiswi  Kemal Ozkan alisema anaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuweka kipaumbele katika kujali maslahi ya watumishi na si makampuni na kuwawezesha wafanyakazi katika sekta ya madini na mafuta kufanya kazi katika mazingira mazuri.

by: madini

Latest News
Biteko atoa wito Mabenki ya ndani kuungana kukope…

Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…

by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.

Ukusanyaji wa Maduhuli Sekta ya Madini Wafikia As…

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…

by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.

Aliyoyasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Adol…

’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…

by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.

Tume ya Madini Yaagizwa Kutafuta Masoko

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…

by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.

Read News
Contact Us
Permanent Secretary,
Ministry of Minerals,
Madini Street,
Government City, Mtumba
P. O. Box 422,
Dodoma, Tanzania
Email: ps@madini.go.tz
Copyright©2021 Ministry of Minerals