Tarehe : Sept. 23, 2019, 6:37 a.m.
Asteria Muhozya, Boaz Mazigo na Greyson Mwase Geita
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kutokana na kuwepo mfumo rasmi wa mapato ya madini yanayotokana na uanzishwaji wa masoko ya madini na Vituo Vidogo vya Ununuzi katika mikoa mbalimbali nchini.
Ameyasema hayo wakati kamati hiyo ilipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel wakati wa ziara yao mkoani humo inayolenga kuangalia namna masoko ya madini yanavyoendeshwa pamoja na kuangalia Maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini yanayoendelea mkoani humo katika Viwanja vya CCM Kalangalala.
Aidha, ameupongeza mkoa wa Geita kutokana na kuweka mazingira mazuri ya uendeshaji wa soko la madini ikiwemo mwamko mkubwa wa wadau wa madini wanaotumia soko hilo na kueleza kuwa, soko hilo ni la mfano mzuri wa masoko huku biashara kubwa ya madini ya dhahabu inaendelea kufanyika vizuri sokoni hapo.
Ameongeza kuwa, masoko hayo yamewezesha kupatikana kwa mapato ambayo kabla ya kuanzishwa kwa masoko fedha nyingi zilikuwa zikipotea kutokana na tabia za utoroshaji madini hali ambayo hivi sasa inadhibitiwa na uwepo wa masoko hayo.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti ameutaka mkoa huo kuangalia namna masuala ya Ulinzi na Usalama yanavyosimamiwa katika uendeshaji wa masoko hayo na kueleza kuwa, yapo malalamiko ambayo yametolewa ikiwemo ucheleweshaji wa muda wa kufungua masoko hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa yapo mapinduzi makubwa yaliyofanywa mkoani humo ambayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Sekta ya madini yakiwemo masuala yanayohusu huduma za Afya na Elimu.
Pia, ameieleza kamati hiyo kuwa, wachimbaji mkoani humo wanapata hamasa ya kuyatumia masoko hayo hali ambayo inapelekea kupata bei halisi ya dhahabu ikiwemo hamasa ya kuanzishwa kwa biashara mbalimbali ambazo zimechangiwa na uwepo wa masoko.
Pia, Mkuu huyo wa Mkoa ameeleza kuhusu mpango wa mkoa huo wa kuwa na eneo rasmi la shughuli za maonesho ambayo lengo ni kufanywa Kimataifa. Mkuu wa Mkoa alisema hayo wakati akijibu hoja ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ambaye ameshauri kuhusu maonesho hayo kimataifa zaidi.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo ameupongeza mkoa huo kwa kuwa na soko linalongooza nchini kwa kuzalisha na kuuza madini likifuatiwa na soko la Madini Chunya.
Naibu Waziri ameongeza kuwa, ni soko linaloongoza kwa kukusanya mrabaha wa serikali ambapo hivi sasa zaidi ya Shilingi Bilioni 2 zinakusanywa kwa mwezi sokoni hapo.
Akizungumzia mauzo ya Soko la Madini Chunya amesema hivi sasa soko hilo linauza hadi kilo 150 kutoka kilo 20 na hivyo kutumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji wote na wadau wa madini nchini kuyatumia masoko hayo na kutoyaogopa.
Pia, Naibu Waziri amezuia kukamatwa kwa wadau wote wa madini wanaofuata Sheria na taratibu katika kuyatumia masoko hayo na kuwataka waachwe wafanye shughuli zao.
Akijibu hoja iliyotolewa na wadau wa madini sokoni hapo kuhusu soko hilo kufanya kazi hadi siku ya Jumapili, Naibu Waziri amesema Wizara kupitia Tume ya Madini na Mkoa wa Geita utaangalia namna ya kulifanyia kazi suala hilo na kuongeza kwamba, tayari Wizara imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya hivyo upungufu wa rasilimali watu utafanyiwa kazi
Pia, Naibu Waziri ameupongeza Mkoa huo kuwa na ubunifu wa hali ya juu na kuulezea kuwa, unaibeba Sekta ya Madini. Pia, ameipongeza Kamati hiyo kutokana na namna inavyoishauri Wizara jambo ambalo linaiwezesha sekta kusonga mbele.
Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda akizungumza wakati wa ziara hiyo amesema kwamba wadau wote wanapokelewa sokoni hapo ikiwemo wachimbaji wasiokuwa kwenye mfumo rasmi. Aidha, ameongeza kuwa, kwa wateja wasiojua kusoma na kuandika wanaofika katika soko la madini kwa ajili ya kupata huduma, wanasaidiwa na maafisa wa Tume ya Madini waliopo kwenye soko hilo namna zuri ya kuweka taarifa zao kwenye nyaraka mbalimbali zinazotumika kwenye ofisi hiyo.
Mbali na Kamati hiyo kutembelea soko la Madini Geita, pia imetembelea maonesho ya madini. Aidha, katika ziara hiyo, Wajumbe hao wa Kamati wamekabidhiwa Mwongozo wa Uwekezaji wa mkoa huo uliozinduliwa wakati wa ufunguzi wa Maonesho hayo Septemba 22, 2019, na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.