Tarehe : Sept. 29, 2022, 12:51 p.m.
Yaomba kufanyika Tafiti za Kina, mwenendo wa makusanyo kichocheo
Na Asteria Muhozya, Tabora
Kutokana na mwenendo mzuri wa makusanyo ya Serikali yanayotokana na rasilimali Madini, Mkoa wa Tabora umeiomba Wizara ya Madini kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania(GST) kufanya tafiti za kina mkoani humo ili kubaini maeno yenye viashiria vya madini kwa lengo la kuongeza wigo wa uzalishaji hususan dhahabu.
Imebainishwa kuwa, tangu kufungwa kwa uliokuwa Mgodi Mkubwa wa uchimbaji madini wa Resolute ambao ulikabidhiwa rasmi kwa kilichokuwa Chuo cha Madini mwaka 2014, mkoa huo haujabahatika kuwa na mgodi mwingine mkubwa au wa kati na hivyo shughuli za madini kwa kiasi kikubwa kufanywa na wachimbaji wadogo wa madini.
Kutokana na makusanyo mazuri yanayotokana na shughuli za uchimbaji mdogo, mkoa huo umeona ipo haja kwa Wizara kusaidia kufanyika kwa tafiti za kina ili kuuwezesha mkoa huo kuongeza kiwango cha uzalishaji madini ikiwemo kuhamasisha uwekezaji.
Hayo yamebainisha kwa nyakati tofauti na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dkt. Batlida Burian na Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Tabora Mayigi Makolobela wakati wa kikao baina yao na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ambaye yupo mkoani humo kwa ajili ya kutembelea shughuli za madini, kuangalia maendeleo na shughuli hizo mkoani humo pamoja na kufahamu changamoto zilizopo katika sekta ya Madini na kufahamiana na watumishi.
Akitoa taarifa ya shughuli za Madini kwa mkoa huo, Makolebela amemweleza Dkt. Kiruswa kuwa, kufikia mwezi Septemba , 2022, ofisi hiyo imekusanya kiasi cha Shilingi 1,549,325,421.17 sawa na asilimia 24.14 ya lengo la mwaka na kuongeza kwamba, lengo la makusanyo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 ni shilingi 6,419,008,300.80.
Makolobela ameongeza kwamba, katika Mwaka wa Fedha 2021/22 ofisi hiyo ilikusanya shilingi 5,672,557,571.89 sawa na asilimia 126.10 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi 4,500,000,000 na kueleza kuwa, mapato hayo yanatokana na shughuli za uchimbaji mdogo.
Akizungumzia mwenendo wa Soko la Madini amesema masoko hayo yamesaidia ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwani takribani asilimia 80 ya makusanyo ya mkoa huo yanatokana na soko la madini.
Akizungumzia mikakati ya kufikia malengo ya makusanyo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, amesema ofisi hiyo imejipanga kuimarisha vyanzo vya mapato hususan makusanyo ya madini ya ujenzi kwa wilaya zote za mkoa huo, kuwaelimisha wachimbaji wadogo kufanya uchimbaji wa kisasa kwa kushirikiana na wawekezaji wanaoonesha nia ya kufanya hivyo, kuendelea kudhibiti utoroshaji wa madini katika maeneo yote ya uchimbaji hususuan dhahabu.
Ameitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuendelea kuimarisha ukaguzi wa migodi na kutatua kero zinazoweza kusababisha uzalishaji kupungua na kufuatilia madeni ya miradi ya Tanroads ambayo haijalipiwa mrabaha na ada ya ukaguzi.
Kwa upande wake, Dkt. Burian amesisitiza kuhusu kufanyika kwa tafiti za kina kuuwezesha mkoa huo kupata wawekezaji wapya wakiwemo wakubwa kutokana na viashiria vya uwepo wa kiasi kikubwa cha rasilimali madini ambao ofisi ya madini imebainisha na kuitaka wizara kulifanyia kazi suala la Mfumo wa maombi ya Leseni kwani umeonekana kuwa na changamoto kwa waombaji.
Akijibu baadhi ya maombi na changamoto zilizotolewa, Naibu Waziri Dkt.Kiruswa amesema tayari wizara imefanya jitihada mbalimbali za kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwaunganisha na taasisi za fedha ili kuwawezesha kupata mikopo na vifaa kuwawezesha kuchimba kwa tija.
Pia, ameongeza kuwa, wizara inatambua kwamba, uwekezaji unategemea taarifa za jiolojia hivyo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kushirikiana na GST yanafanya juhudi mbalimbali za kuongeza wigo wa kufanya tafiti za gharama nafuu kuwezesha kufikiwa kwa maeneo mengi zaidi yenye viashiria vya madini ili kuwawezesha wachimbaji kuchimba pasipo kubahatisha.
Kutokana na juhudi hizo za Serikali, amewataka wachimbaji wadogo mkoani humo na maeneo mengine kujiunga katika vikundi ili taasisi hizo ziwafikie kwa urahisi na kwa gharama nafuu na kuongeza kuwa, wizara imeweka mkakati wa kuwatengea maeneo wachimbaji wadogo ambayo tayari yana taarifa za kijiolojia.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameupongeza mkoa huo kutokana na makusanyo mazuri ya maduhuli licha ya shughuli hizo kwa kiasi kikubwa kufanywa na wachimbaji wadogo.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.