Tarehe : May 9, 2019, 4:40 a.m.
Waziri wa Madini, Doto Biteko amesema, katika kuhakikisha kwamba mchango wa sekta ya madini unaifikisha nchi kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025, masoko ya madini ni muhimu.
Ameyasema hayo leo, alipokuwa akizindua soko la madini la Mkoa wa Mwanza ambapo amewataka viongozi mbalimbali wa serikali katika ngazi zote kushiriki kikamilifu katika kutekeleza mipango iliyowekwa na Serikali kupitia Wizara yake ili kuifikisha nchi katika uchumi huo wa kati.
Biteko amesema, wizara imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao cha Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kilichofanyika mwezi Januari, 2019 Jijini Dodoma kikao kilicholenga kujenga uelewa wa pamoja juu ya maudhui ya kanuni wa uanzishwaji masoko ya madini nchini.
Aliendelea kusema, katika kuelekea uanzishwaji wa masoko ya madini nchini ulioanza mapema mwezi Februari, wizara ilifanikiwa kufanya mafunzo kwa Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi pamoja na Makatibu Tawala wa Wilaya.
Pamoja na jitihada hizo, Wizara ilifanikiwa kufanya Mkutano Mkubwa wa kisekta mwishoni mwa mwezi Januari 2019 na kupokea maoni mbalimbali ya wadau yaliyopelekea Serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya mwaka 2019 iliyohusisha utungwaji wa kanuni za masoko kwa ajili ya kuanzishwa masoko ya madini.
Aidha, Biteko amesema serikali ilikubali ombi la wadau la kupunguza utitiri wa kodi na tozo mbalimbali kwa wachimbaji wadogo na kuamua kufuta baadhi ya kodi hizo ikiwemo kodi ya zuio (withholding tax) pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa wachimbaji wadogo.
Akizungumzia historia ya uanzishwaji wa soko la madini mkoani Mwanza, Biteko alisema ilianza mnamo mwaka 2018 wakati wizara ilipounda kamati maalum kwa lengo la kubaini sababu ya utoroshwaji wa madini hasa madini ya dhahabu na vito.
Biteko anasema pamoja na hilo kamati ilibaini kuwa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali zilizokuwa zikitozwa kwa wachimbaji wadogo wa madini ni sababu nyingine iliyochangia utoroshwaji wa madini nchini na kukiri chimbuko la uanzishwaji wa masoko ya madini kuwa ni Mwanza kupitia kamati hiyo.
“Uzinduzi wa soko hili unatoa majibu kwa maswali ya wananchi kuhusu changamoto ya utoroshwaji wa rasilimali madini ambayo imedumu kwa muda mrefu” Biteko alikazia.
Aidha, Biteko amewataka wadau wote katika mnyororo mzima wa uendeshaji wa masoko ya madini kutimiza wajibu wao kwa uzalendo wa kiwango kinachostahili.
Kwa upande wake katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila amewataka viongozi wa serikali kushiriki kikamilifu katika kusimamia rasilimali madini inayopatikana nchini.
Akielezea idadi ya masoko yaliyofunguliwa mpaka sasa, Prof. Msanjila alisema ni masoko ya madini 13 na siku ya leo masoko ya madini manne yanafunguliwa likiwemo la Mwanza, Kagera, Iringa na Songwe wakati taratibu za kukamilisha zoezi hilo kwa mikoa iliyosalia nchi nzima zikiendelea.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela alisema, Mkoa wa Mwanza unazalisha madini ya dhahabu na madini ya ujenzi kwa kiasi kikubwa katika wilaya ya Kwimba na Misungwi na kiasi kidogo katika maeneo ya Sengerema. Alikiri uwepo wa uzalishaji wa madini ya almasi kwa kiwango kidogo katika maeneo ya Mabuki na Manangwa wilayani Misungwi.
Mongela amebainisha kuwa wananchi wa mkoa wa Mwanza wana imani kuwa usimamizi mzuri wa sekta ya madini utaipelekea nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Akihitimisha hotuba yake, Mkuu wa Mkoa Mongela alisema mkoa wake utahakikisha madini yote yanayozalishwa yanauzwa katika soko lililofunguliwa kwa kuzingatia sheria, kanuni pamoja na miongozo ya mbalimbali ya kisekta.
Amesema kuanzishwa kwa soko la madini Mwanza, ni fursa ya kipekee kwani Mkoa wa Mwanza utakuwa ni kitovu cha biashara ya madini katika ukanda wa ziwa victoria kutokana na mazingira yake kijiografia pamoja na miundombinu.
Akizungumza kwa niaba ya wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, Makono Kaniki aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Madini kuongeza watumishi katika masoko yaliyofunguliwa ili kurahisisha zoezi zima la uuzaji na ununuzi wa madini.
by: madini
Waziri wa Madini, Doto Biteko ameyataka Mabenki ya ndani kushirikiana ili kuweza kuzikopesha kampun…
by: madini on: April 23, 2021, 5:11 a.m.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 202…
by: madini on: April 28, 2021, 12:51 p.m.
’Nimeona Nyuso Zenye Furaha , Amani na Utulivu’’ Ninayo furaha kuwa nanyi hapa ili tuanze safari hi…
by: madini on: Jan. 10, 2022, 2:55 p.m.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameiagiza Tume ya Madini kutafuta Masoko ya wanunuzi wa…
by: madini on: Jan. 30, 2022, 9:32 a.m.